Na Stella Herman, Shinyanga
Watoto wa kike wanaohudumiwa na Shirika la Agape Aids Control Programme katika Kituo cha Chibe, Manispaa ya Shinyanga, wameungana na mdau wa maendeleo na Diwani wa Viti Maalum, Veronica Masawe, kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.
Masawe amefika katika kituo hicho leo Septemba 15, 2026, ambapo amejumuika na watoto hao na kusherehekea pamoja nao siku hiyo muhimu katika maisha yake.
Akizungumza wakati wa sherehe hiyo, Masawe amesema ameamua kutumia siku yake ya kuzaliwa kwa kwenda katika kituo hicho ili kujumuika na watoto na kufurahi pamoja.
Mbali na kujumuika nao, Masawe ametoa vyakula kwa watoto hao ili waweze kusherehekea pamoja na kufurahia siku hiyo.
“Nimefurahi sana kufika katika kituo hiki na kujumuika na watoto hawa katika siku yangu ya kuzaliwa. Nawaomba mpokee kidogo nilichowaletea ili tufurahi pamoja, ninyi ni sehemu ya jamii,” amesema Masawe.
Watoto hao wanahudumiwa na kituo hicho baada ya kukumbwa na madhara mbalimbali ya ukatili wa kijinsia, huku kituo kikiwasaidia kuendelea na elimu na kufikia ndoto zao.
Masawe amewahimiza watoto hao kusoma kwa bidii, kuzingatia nidhamu, kujituma na kutumia ipasavyo elimu wanayoipata ili waweze kutimiza ndoto zao.
Katika hatua nyingine Masawe amewaomba wadau mbalimbali wajitokeze na kuwasaidia watoto hao katika Kituo cha Agape kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya watoto wenzake, Anna Francis ametoa shukrani kwa Masawe kwa zawadi na vyakula walivyopatiwa, akisema kitendo cha kwenda kujumuika nao kimewapa faraja na kuwafanya wajione kuwa wanathaminiwa na jamii.