.jpeg)
Na mwandishi wetu-shinyanga,
Mamlaka ya Mapato Tanzania (Tanzania Revenue Authority-TRA) Mkoa wa Shinyanga imewapatia wafanyabiashara wa mkoa huo elimu kuhusu mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi yaliyoanza kutekelezwa kufuatia marekebisho yaliyoidhinishwa na Serikali kuanzia Juni 30, 2026.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Agosti 20, 2026, Meneja wa Msaidizi Huduma kwa Mlipa kodi Mkoa wa Shinyanga,Ramadhan Sengo alisema Mamlaka hiyo imewaalika wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo ili kuwapatia elimu ya kina kuhusu mabadiliko ya sheria na kuwapa fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu wa kodi.
Alisema elimu hiyo ni muhimu katika kujenga uelewa wa pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika suala la ulipaji na ukusanyaji wa kodi.
“Kwa pamoja, mafunzo haya ni muhimu katika kuongeza jitihada za wafanyabiashara na taasisi kwa pamoja ili kusaidia Taifa letu kuwa na uwezo wa kukusanya kodi kwa ajili ya maendeleo. Tumieni fursa hii kuuliza maswali yatakayotupa uelewa na kutusaidia kujua mambo mbalimbali kupitia wataalamu wa Mamlaka ya mapato Tanzania,” amesema Sengo.
.jpeg)
.jpeg)
Afisa Mkuu Msimamizi wa kodi-Mamlaka ya Mapato mkoa wa Dar es salaam,Abdalah Seif akitoa maelezo ya mabadiliko ya kodi kwa wafanyabiashara.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Taifa ya biashara Tanzania mkoa wa Shimyanga(TNCC)Tanzania, Thabiti Mgeja alisema sekta binafsi ni injini muhimu ya maendeleo ya Taifa na kwamba ushirikiano kati ya Serikali na wafanyabiashara ni muhimu katika kujenga mazingira bora ya biashara.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeonyesha nia ya kuimarisha ukusanyaji wa kodi kwa kushirikisha wananchi na kutoa elimu kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi.
“Tunashukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuleta mabadiliko chanya katika mfumo wa kodi kwa wafanyabiashara, hatua ambayo inalenga kusaidia ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya maendeleo ya Taifa,” amesema Mgeja.
.jpeg)
Wafanyabiashara hao pia waliomba TRA kuendelea kushirikisha taasisi nyingine zinazohusiana na shughuli zao, ikiwemo TANROADS, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), TARURA na Halmashauri, katika kutoa elimu ya pamoja kuhusu masuala ya kodi na majukumu mbalimbali yanayowahusu wafanyabiashara.
Walisema ushirikishwaji wa taasisi hizo utasaidia kupunguza mkanganyiko unaoweza kujitokeza kwa wafanyabiashara wanapotekeleza majukumu yao ya kikodi na majukumu mengine yanayohusiana na uendeshaji wa biashara.
Christopher Ringo, Mkurugenzi wa Lyakale Civil Engineering, aliomba TRA Mkoa wa Shinyanga kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa watumishi wa TANROADS na TARURA, akisema elimu hiyo itasaidia kuongeza uelewa na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya kikodi kwa wakandarasi kutokana na kuchelewa kwa malipo yao.
Mabadiliko ya sheria za kodi yaliyoelezwa katika mafunzo hayo yanahusu maeneo mbalimbali, ikiwemo uuzaji wa mali, mazao ya misitu, ushuru wa uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, uendeshaji wa kampuni za madini, viwango vya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), wajibu wa waajiri kuzingatia Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN), mirahaba ya malipo kwa timu za mpira wa miguu , biashara zinazofanyika kupitia mitandao, kodi kwa vyombo vya usafiri wa abiria, wajibu wa kulipa kodi pamoja na kodi zinazohusiana na michezo ya bahati nasibu.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa katika mafunzo hayo, marekebisho hayo yamegusa baadhi ya vifungu vya sheria mbalimbali za kodi, ikiwemo Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Sheria ya Ushuru pamoja na masharti yanayohusu Capital Gains Tax, kwa lengo la kuimarisha mfumo wa ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya Serikali.
Wafanyabiashara wameendelea kusisitiza umuhimu wa Serikali na taasisi zake kutoa elimu ya mara kwa mara kuhusu mabadiliko ya sheria ili kuhakikisha walipa kodi wanapata uelewa sahihi wa wajibu wao na kuepuka makosa yanayoweza kusababisha migogoro au adhabu za kikodi.
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)