` MADIWANI KISHAPU WAJADILI UWAJIBIKAJI WA MENEJIMENTI KWA MWAKA WA FEDHA 2025/2026, WAPONGEZA KASI UKUSANYAJI MAPATO

WANDAMAN HOTEL

MADIWANI KISHAPU WAJADILI UWAJIBIKAJI WA MENEJIMENTI KWA MWAKA WA FEDHA 2025/2026, WAPONGEZA KASI UKUSANYAJI MAPATO

 

MADIWANI KISHAPU WAJADILI UWAJIBIKAJI WA MENEJIMENT KWA MWAKA WA FEDHA 2025/2026 WAPONGEZA KASI UKUSANYAJI MAPATO

Na Mwandishi Wetu, KISHAPU

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu limejadili taarifa ya utendaji na uwajibikaji wa Menejimenti ya Halmashauri katika mwaka wa fedha 2025/2026 huku wakipongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Kikao hicho kilifanyika Septemba 10,2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.

Katika kikao hicho, taarifa za shughuli za utendaji wa Menejimenti ziliwasilishwa na wakuu wa idara na vitengo, ambapo madiwani walipata nafasi ya kujadili kwa kina na kutoa maelekezo kwa ajili ya kuimarisha ufanisi wa Halmashauri kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Josephat Limbe, amewashukuru madiwani kwa kujadili kwa kina taarifa zilizowasilishwa na kuahidi kuendelea kushirikiana kwa pamoja.

“Yapo mafanikio ambayo ninakiri kama Mwenyekiti, kwa namna ambavyo tumeshirikiana kwa pamoja na Menejimenti,” amesema Limbe.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Emmanuel Johnson, amewashukuru madiwani akisema majadiliano hayo yaliyotokana na taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya idara na vitengo na kwamba yamewapa mwelekeo mpya kama Menejimenti wa kujitathmini na kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa, ili kuimarisha ustawi wa Halmashauri.

Naye Diwani wa Kata ya Sekebugoro Fredinand Mpogomi, kwa niaba ya madiwani, ametoa pongezi kwa Halmashauri kutokana na taarifa iliyowasilishwa na Kitengo cha Fedha na Uhasibu, ambayo ilibainisha kuongezeka kwa kiwango cha makusanyo ya mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.

“Halmashauri yetu imepiga hatua katika makusanyo ya mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo tulifikia asilimia 93 tunapaswa tujipongeze kwa hili, na tujipange sasa kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ili tufikie asilimia 100,” amesema Mpogomi.

TAZAMA PICHA👇👇
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Josephat Limbe akizungumza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Emmanuel Johnson akizungumza.
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Ibrahimu Makana akizungumza.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464