
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu amebainisha kuwa mfuko huo utaratibiwa kupitia Benki ya CRDB na utamsaidia mtu aliyepata kazi nje kuwa na amani na uhakika wa kukamilisha safari yake
Hii ni sehemu ya mikakati ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuleta utulivu kwa vijana kwa kuhakikisha kuwa ukosefu wa nauli au gharama za awali hauwi kikwazo cha wao kupata maisha bora kupitia ajira za nje.
Mbali na mfuko huo, serikali inaanzisha kituo maalumu cha kutekeleza mitaala ya kuwanoa zaidi Watanzania wanaosaka kazi nje.
Kabla ya kuondoka, vijana watapitishwa katika mchakato wa "kupigwa brashi" ili waweze kuingia kwenye soko la ushindani wakiwa na ujuzi na uelewa wa kutosha wa kazi zao kwa mujibu wa mikataba yao.
Hata hivyo,Naibu Katibu Mkuu (Kazi), Zuhura Yunus, ameeleza kuwa kuondoka kwa vijana hao 109 ni utekelezaji wa Sera ya Ajira ya mwaka 2018, inayolenga serikali kuwezesha kupatikana kwa ajira zenye staha kwa wananchi wake.
Pia Waziri Sangu amewataka vijana kuwa na nidhamu na uaminifu wanapokuwa kazini huko ughaibuni. Amesema kuwa kijana mmoja akiwa mwizi au mvivu, haumii yeye pekee, bali anafunga milango kwa Watanzania wengine kwani sifa ya nguvu kazi ya Tanzania itashuka.
Alisisitiza kuwa ili kuleta uchumi shindani kuelekea dira ya 2050, Watanzania vijana wanaoenda ughaibuni wanapaswa kuwa mabalozi wema wanaovutia waajiri wa kimataifa kuendelea kuajiri kutoka Tanzania.
Vilevile, Meneja Uhusiano wa NSSF, Lulu Mengele, amewataka vijana hao kujiunga na hifadhi ya jamii kabla ya kuondoka. Kupitia NSSF, vijana wanaofanya kazi nje wataweza kuwekeza akiba zao, kulinda familia zao kupitia bima ya matibabu, na kuwa na uhakika wa maisha pindi mikataba yao itakapomalizika.
Huu ni utaratibu wa kimkakati wa kuhakikisha kuwa kipato kinachopatikana nje kinatumika kuimarisha maisha ya familia za vijana hawa na kuchochea uwekezaji nchini.