Na Emmanuel Jonson, NYANDOLWA
Serikali Mkoa wa Shinyanga imetoa kibali kwa kampuni ya HHH and Partners kuendelea na shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo la Nyandolwa, baada ya leseni zake kusimamishwa kufuatia ajali iliyotokea Agosti 11, 2025 na kusababisha mafundi 25 kufukiwa wakati wakifanya ukarabati wa maduara ya Kikundi cha Mchapakazi Nyandolwa.
Akitoa kauli ya Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya ukaguzi wa kina uliofanywa na wataalamu wa Serikali wakiongozwa na Mkaguzi Mkuu wa Migodi nchini, Hamis Kamando.
Amesema baada ya tathmini ya kina, Serikali imeridhika kuwa kampuni ya HHH and Partners inaweza kuendelea na uzalishaji kwa kuzingatia maelekezo yote ya kiusalama yaliyotolewa na wataalamu.
“Timu ya wataalamu wa Serikali ilifika Nyandolwa kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ajali ya Agosti 11, 2025. Baada ya ukaguzi huo, ilishauri hatua mbalimbali za kuchukuliwa ili kuhakikisha usalama wa wachimbaji,” amesema Mhita.
Kwa upande wa Kikundi cha Mchapakazi, Mhita ameeleza kuwa kati ya maduara 66 yaliyokaguliwa, 44 yalibainika kuwa hatarishi na hivyo kufungwa, huku maduara 22 yakiruhusiwa kuendelea na uzalishaji baada ya kukidhi vigezo vya usalama.
Aidha, kwa upande wa HHH and Partners, amesema kampuni hiyo ilikuwa na maduara 26, ambapo 19 yalionekana kuhatarisha usalama wa wachimbaji na kufungwa, na saba pekee ndiyo yameruhusiwa kuendelea na uzalishaji mara moja baada ya kutekeleza maelekezo ya wataalamu.
Mhita amesisitiza kuwa maduara 22 a kikundi cha Mchapakazi ambayo yameelekezwa kufanyiwa ukarabati ili kukidhi vigezo ukarabati wake unapaswa kufanyika haraka kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu ili yaweze kukaguliwa tena na kuruhusiwa kuendelea na uzalishaji.
Pia amewataka wamiliki wa leseni kufuata taratibu na miongozo ya usalama hatua kwa hatua ili kuzuia maafa kama hayo yasijirudie.
Kwa upande wake, Mkaguzi Mkuu wa Migodi, Hamis Kamando, amesema ajali nyingi migodini husababishwa na uzembe wa wamiliki, akisisitiza umuhimu wa kufanya ukaguzi na matengenezo ya mara kwa mara ili kuimarisha usalama na kulinda nguvu kazi ya taifa.
Naye Meneja wa Leseni ya HHH and Partners, Hamad Hussein, ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuufungulia mgodi huo. Amesema hatua hiyo itasaidia kurejesha ajira zilizokuwa zimesimama tangu kusimamishwa kwa uzalishaji.
Mtumishi wa kampuni hiyo, Paschal Andrea, amesema kufunguliwa kwa mgodi huo kutaongeza fursa za ajira kwa vijana wa eneo hilo na kusaidia kurejesha kipato kwa familia nyingi zilizokuwa zimeathirika na kusimamishwa kwa shughuli za uchimbaji.
Mgodi huo ulifungwa kufuatia ajali ya kuporomoka kwa maduara, na sasa umefunguliwa tena kwa masharti ya kuzingatia kikamilifu kanuni na taratibu za usalama zilizowekwa na Serikali.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464




