` ELIMU YA JUU, UZALISHAJI WA NDANI NA NGUVU YA SHILINGI

ELIMU YA JUU, UZALISHAJI WA NDANI NA NGUVU YA SHILINGI

Wapiga ramli na wachochezi nchini wanaoshangilia misukosuko wanapaswa kuzinduka na kutambua kuwa Tanzania inajenga ngome yake ya kiuchumi kupitia uwekezaji wa kudumu katika vichwa vya vijana wake. 

Profesa Adolf Mkenda na Serikali ya Awamu ya Sita wameamua kuweka fedha kwenye elimu inayozalisha badala ya elimu ya sifa, na hii ndiyo siri ya mafanikio ya sera za fedha nchini. Shilingi yetu inapata thamani kwa sababu inaungwa mkono na nguvu kazi inayopikwa kulinda na kuzalisha thamani hiyo ndani ya nchi.

Mageuzi haya yanayofanyika katika sekta ya elimu, sayansi na teknolojia ni kielelezo tosha cha jinsi serikali inavyotumia rasilimali zake kimkakati ili kuimarisha uchumi kuanzia ngazi ya chini. 

Kupitia mradi wa HEET uliogharimu Shilingi trilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya elimu ya juu nchi nzima, serikali inatengeneza mazingira ambayo mwananchi wa kawaida anaanza kunufaika kupitia mzunguko wa fedha unaotokana na ujenzi huo. Mafundi, wasambazaji wa vifaa na vibarua mitaani wanapata kipato cha moja kwa moja, huku vijana wakitayarishwa kuwa wazalishaji badala ya kuwa walaji au watafuta ajira pekee.

Kiini cha mafanikio haya ya kiuchumi kinajikita kwenye uzalishaji ambao ndio nguzo ya sarafu imara. Serikali inapowekeza kwenye Taasisi ya Sayansi za Bahari kule Zanzibar, inageuza rasilimali za bahari kuwa fursa za kiuchumi kupitia utafiti na utaalamu wa ndani. 

Hali hii inapunguza gharama za kuagiza wataalamu kutoka nje ya nchi ambazo zingetulazimu kutumia fedha za kigeni. 

Matokeo yake ni kuifanya Shilingi ya Tanzania kuwa shindani kwa sababu inategemewa na huduma na bidhaa zinazozalishwa na Watanzania wenyewe.

Sera za fedha nchini sasa zinafanikiwa kwa sababu zinaambatana na uwekezaji kwenye miundombinu ya binadamu. Elimu ya juu inayozalisha ujuzi inasaidia kudhibiti mfumuko wa bei kwa kupunguza utegemezi wa nje na kuimarisha uwezo wa ndani wa kujitegemea. Hii ndiyo njia pekee ya kuelekea Dira ya 2050 ikiwa na uchumi shindani unaotokana na maarifa. 

Ni lazima ifahamike kuwa nguvu ya taifa lolote kiuchumi haitokani na kelele za nje, bali inatokana na uwezo wa vijana wake kujiajiri, kuzalisha na kuleta utulivu wa kijamii kupitia sayansi na teknolojia kama anavyosisitiza Profesa Mkenda.

Watanzania na hasa vijana wanatakiwa kuunganisha nukta ambazo mara nyingi watu wanashindwa kuziona na kushabikia uasi wakisahau kwamba kuna uhusiano mkubwa wa amani na kujipatia elimu ya juu, uzalishaji wa ndani, na nguvu ya Shilingi ambayo hutengeneza uchumi wa mtu mmmoja mmoja na kisha taifa.

Kiukweli uzalishaji ndio uhai wa sarafu: Huwezi kuwa na fedha imara kama nchi yako haizalishi wataalamu. Profesa Mkenda anapozungumzia trilioni moja ya HEET, hapo anazungumzia kutengeneza "viwanda vya akili" ambavyo vitazalisha bidhaa na huduma, na hivyo kuipa thamani Shilingi yetu bila kutegemea misaada na huili linawezekana kwenye utulivu na hakuna ghasia wala uasi.

Ndio kusema katika siasa za kijiopolitika (kama tulivyoona kwenye mfano wa Venezuela na Greenland), nchi yoyote isiyo na utulivu wa ndani wa kiuchumi ni rahisi kuyumbishwa. Kwa kuwekeza kwenye elimu inayozalisha ajira (kujiajiri), serikali inakata mzizi wa malalamiko na uchochezi kwa kutengeneza vijana wenye tija. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464