` KATAMBI ATOA ONYO KWA MKANDARASI NGUZO NANE–MWAWAZA, ASEMA “TUKO RADHI KUVUNJA MKATABA”

KATAMBI ATOA ONYO KWA MKANDARASI NGUZO NANE–MWAWAZA, ASEMA “TUKO RADHI KUVUNJA MKATABA”


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mheshimiwa Paschal Patrobas Katambi, akiwa katika eneo la mradi wa  ujenzi wa barabara ya lami kutoka Nguzo Nane kuelekea Hospitali ya Mwawaza. Picha na Noel Kasili  
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mhe. Paschal Patrobas Katambi, akizungumza wakati akitembelea mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Ibadakuli uliopo katika Manispaa ya Shinyanga.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mhe. Paschal Patrobas Katambi, akizungumza wakati akitembelea mradi wa ujenzi Stendi Mpya ya Mabasi Kizumbi katika Manispaa ya Shinyanga

Na Paschazia Charles - Shinyanga

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mheshimiwa Paschal Patrobas Katambi, ameonesha kutoridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka Nguzo Nane kuelekea Hospitali ya Mwawaza, akieleza wazi kuwa maendeleo ya mradi huo hayalingani na fedha zilizokwisha kutolewa na Serikali, na kusisitiza kuwa hakuna muda wa nyongeza utakaotolewa kwa mkandarasi iwapo hatatimiza wajibu wake kwa wakati.

Mhe. Katambi ametoa kauli hiyo leo  Februari 23,2026 alipofanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Jimbo la Shinyanga Mjini, ikiwemo mradi wa barabara ya lami Nguzo Nane–Mwawaza, ujenzi wa Stendi Mpya ya Mabasi Kizumbi, pamoja na mradi wa ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Ibadakuli mkoani Shinyanga.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi ya barabara ya Nguzo Nane–Mwawaza na Stendi ya Mabasi Kizumbi inayotekelezwa na mkandarasi kutoka Kampuni ya SIHOTECH Engineering, Mheshimiwa Katambi amesema utekelezaji wa miradi hiyo unasuasua. 

Ameeleza kuwa hadi sasa ujenzi wa barabara ya Mwawaza umefikia asilimia 13, ujenzi wa Stendi Mpya ya Mabasi Kizumbi umefikia asilimia 32, huku ujenzi wa jengo la TARURA ukiwa umefikia asilimia 35.

Kutokana na hali hiyo, Katambi amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji kwa kufanya kazi kwa haraka na weledi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati kama mkataba unavyoelekeza, akisisitiza kuwa hakutakuwa na muda wa nyongeza.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mhe. Paschal Patrobas Katambi, akizungumza wakati akitembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Nguzo Nane kuelekea Mwawaza katika Manispaa ya Shinyanga.

“Hali inayoonekana hapa hairidhishi kabisa, nilitegemea utekelezaji uwe umefikia thamani ya pesa mliyotanguliziwa ya Sh. 3.9 bilioni, mkandarasi unatakiwa kufanyakazi usiku na mchana kukamilisha kazi kwa muda uliowekwa katika mkataba hakuna muda utakaoongezwa, tuko radhi kuvunja mkataba kama mambo hayaeleweki” ,amesema Katambi.

Aidha, Mhe. Katambi amesisitiza kuwa mkandarasi wa miradi ya barabara ya Mwawaza na Stendi ya Mabasi Kizumbi anatakiwa kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha miradi hiyo kwa mujibu wa masharti ya mkataba.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mhe. Paschal Patrobas Katambi, akizungumza wakati akitembelea mradi wa ujenzi wa Stendi ya Mabasi Kizumbi.

Katika hatua nyingine, Waziri Katambi ametembelea mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Ibadakuli ambapo ameonesha kufurahishwa na maendeleo ya utekelezaji wake.

 Katambi ameipongeza Kampuni ya China Hennan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) kwa kusimamia vyema mradi huo na kuhakikisha unakaribia kukamilika kwa wakati.
Amesema hadi sasa utekelezaji wa mradi wa uwanja wa ndege wa Mkoa wa Shinyanga umefikia asilimia 95, huku asilimia tano iliyosalia ikihusisha ukamilishaji wa jengo la abiria na majaribio ya vifaa kwa ajili ya kuruhusu ndege kutua nyakati za usiku.

“Utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa uwanja wa ndege wa mkoa wa Shinyanga umefikia asilimia 95 na asilimia tano zilizobaki ni ukamilishaji wa jengo la abiria, na majaribio ya vifaa kwa kutua ndege nyakati za usiku” ,amesema Katambi.

Pamoja na kupongeza hatua iliyofikiwa, Katambi ameishauri kampuni hiyo ya CHICO kutekeleza kwa vitendo ahadi zake kwa jamii, ikiwemo kuwapelekea maji wananchi kama walivyowaahidi, pamoja na kujenga shule ya msingi katika eneo litakaloainishwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri. 
Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza adha kwa wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kufuata huduma ya elimu, na kuwa sehemu ya kurudisha kwa jamii ili kujenga mahusiano mema kati ya mradi na wananchi wanaouzunguka.

Kwa upande wake, Mhandisi Msaidizi wa Kampuni ya SIHOTECH Engineering, Edwine Rwezaula, amesema watajitahidi kufanya kazi kwa weledi na kwa kasi ili kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.

 Ameeleza kuwa tayari wamechukua hatua kadhaa za kuongeza ufanisi, ikiwemo kuongeza idadi ya wafanyakazi, vitendea kazi pamoja na kuongeza muda wa kazi ambapo awali walikuwa wakifanya kazi mchana pekee na sasa wameanza kufanya kazi pia usiku.



Picha na Noel Kasili  
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464