Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA
Diwani wa Kata ya Ilola Kisena Fred Kisena, amelazimika kuchelewa kuhudhuria hitimisho la ziara yake ndani ya kata hiyo, baada ya kukumbwa na changamoto ya ubovu wa miundombinu katika barabara ya Didia–Solwa iliyokatika kutokana na maji, hali iliyosababisha kero kubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Tukio hilo lilitokea katika eneo la dimbwi lililojitokeza barabarani, ambapo Diwani huyo alilazimika kuanza kuwavusha wanafunzi wa shule waliokuwa na hofu ya kusombwa na maji. Alitumia pikipiki kuwavusha wanafunzi hao ili kuhakikisha wanafika salama upande wa pili.
Mbali na kuwasaidia wanafunzi, Kisena pia alishirikiana na wananchi kukwamua bajaji zilizokuwa zimekwama kwenye dimbwi hilo. Bajaji hizo zilikuwa zimebeba mpunga zikielekea Didia kwenye viwanda vya kuchakata mpunga.
Diwani huyo alilazimika kuingia majini pamoja na wananchi na kuanza kusukuma bajaji hizo hadi zilipovuka salama, hatua iliyosaidia kuokoa mali na kuendelea kwa shughuli za kiuchumi.
Akizungumzia hali hiyo, Kisena ametoa wito kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuangalia kwa jicho la pekee dimbwi hilo na kuchukua hatua za haraka.
Ameshauri hali ya dharura itangazwe katika eneo hilo na daraja lijengwe haraka ili kuondoa adha kwa wananchi na wafanyabiashara, akisisitiza kuwa barabara ya Didia–Solwa ni muhimu kwa uchumi wa Wilaya ya Shinyanga DC.
“Barabara hii ni kiungo muhimu cha shughuli za uchumi, hasa usafirishaji wa mazao kama mpunga. Serikali kupitia TARURA ichukue hatua za haraka kuweka daraja ili kuepusha hasara na kuhatarisha maisha ya wananchi,” amesema Kisena.




