` WATANZANIA WAKUMBUSHWA TAHADHARI YA SAMWEL SITTA YA VIONGOZI WA DINI KUELEKEZA WAUMINI KAMA WANASIASA

WATANZANIA WAKUMBUSHWA TAHADHARI YA SAMWEL SITTA YA VIONGOZI WA DINI KUELEKEZA WAUMINI KAMA WANASIASA


Mvutano ulioibuka kufuatia kauli za hivi karibuni za Katibu wa TEC, Padri Charles Kitima, umeibua tena mjadala kuhusu mipaka ya ushiriki wa Taasisi za Dini katika masuala ya utawala na siasa. 

Wachambuzi wanaonya kwamba hatua ya viongozi wa dini kujipambanua kama wanasiasa, badala ya wapatanishi, inahatarisha si tu amani ya nchi, bali pia uhuru wa kiroho na kifikra wa waumini wao.

Kazi ya Kiongozi wa Dini ni kuongoza kiroho na kuimarisha maadili ya umma, si kuamuru Serikali ifanye nini au kuwafanya waumini kutii mwelekeo wa kisiasa wa taasisi zao. Kwa sasa, hali inajirudia, ambapo viongozi hawa wanawaelekeza waumini wao kile wanachotaka kifanyike kisiasa, badala ya kuwapa hekima ya Maandiko na kuacha Serikali itekeleze majukumu yake.


KUTOKA KANISA KWENDA BARAZA LA SIASA

Hatari hii si ngeni katika historia ya nchi. Wakati wa mchakato wa Katiba Mpya, ambapo masuala ya dini na Muungano yaliwekwa mezani, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Hayati Samwel Sitta, alilazimika kutoa tahadhari kali na kukutana na viongozi wakuu wa dini.

Sitta alisisitiza kuwa mchakato wa Katiba ulikuwa wa Kitaifa na haukupaswa kutekwa na ajenda za vikundi vidogo, iwe ni kisiasa au kidini. Lengo kuu lilikuwa kujenga taifa moja lenye misingi ya kisheria inayowakilisha Watanzania wote, bila kujali imani zao.

TAHADHARI YA SITTA: 

Msimamo wa Sitta ulikuja kama onyo dhidi ya makundi yaliyotaka kutumia jukwaa la Katiba kama uwanja wa kupigania maslahi yao, badala ya maslahi mapana ya nchi. Alihangaika kulinusuru Bunge hilo na kuweka wazi kuwa uongozi wa kidini unapovuka mipaka, lengo la kweli la amani hutiliwa shaka.

Kukataa kwa Padri Kitima kutambua wito wa Rais wa maridhiano na kusisitiza kwa bidii Serikali ikiri makosa, kunafanana na hali ya kupuuza wito wa jamii kwa ajili ya uponyaji wa Kitaifa. Kwa kufanya hivyo, kiongozi huyo anajitoa kwenye kiti cha upatanishi na kukalia kiti cha mwanasiasa wa upinzani, akitoa amri kwa Serikali na kwa waumini wake.

Kama alivyoshauri Rais Samia, inahitajika kuacha yaliyopita, na badala ya kuendelea kuitaka Serikali "ikiri", viongozi wa dini wanapaswa kurudi nyuma na kuangalia wajibu wao wa Bibilia: kufanya amani na kuheshimu mamlaka (Warumi 13:1). Kuvaa koti la siasa chafu kwa mgongo wa imani, ni kitendo kinachoweza kuipoteza nchi na kugawanya waumini kwa misingi ya kisiasa, jambo ambalo ni kinyume cha maendeleo.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464