
Kauli ya Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima,imezua taharuki nchini, ikitafsiriwa na wachambuzi wengi kama kauli za uchochezi zaidi kuliko kuponya.
Kauli hiyo wanasema wachambuzi inaonekana kuhalalisha matukio ya ghasia ya Oktoba 29 kwa kuyaita "maandamano" badala ya uhalifu.
Wachambuzi hao wakielezea kuhusu mkutano wake na waandishi wa habari ulioenda mubashara, kwamba mazungumzo yake yalionekana kwenda kinyume na wito wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa maridhiano na amani.
Wachambuzi wameeleza kusikitishwa kwao na namna ambavyo kiongozi huyo, kwa kutumia mgongo wa Kanisa, anajaribu "kum pre-empt Rais" na "kuua ujumbe wa amani" kwa kutoa kauli zake mubashara muda mfupi tu kabla ya Mkuu wa Nchi kufanya mikutano muhimu. Hoja hii inaashiria mlengo na ajenda ya kisiasa.
Kwa mujibu wa maoni ya mtandaoni, baadhi ya wachambuzi wamekumbusha maneno ya Maandiko Matakatifu wakisema: "IMEANDIKWA HERI YAO WAPATANISHI " na hivyo wanamshangaa kiongozi huyo wa kanisa badala ya kujikita kupatanisha anatoa maneno ya kuwasha moto na hivyo kuibua maswali mazito kuhusu wajibu wa Kanisa: je, tunataka kuona taifa letu likitumbukia kwenye shimo la machafuko?
Aidha wachambuzi hao wanasema mdudu hatari anayeitwa udini pia anaonekana kunyemelea kutokana na kauli za kiongozi huyo wa kanisa. Kuhoji kwanini viongozi wenzao wa dini nyingine hawakulalamika mauaji yaliyotokea miaka ya nyuma, kunathibitisha kuwepo kwa uadui unaohama baina ya viongozi wa dini na wafuasi wao, jambo linalotishia umoja na mshikamano wa kitaifa.
Wakati taifa linahitaji uponyaji na kukumbatia amani, wachambuzi wanamtaka Padri Kitima na wenzake kutambua wajibu wao wa kihistoria. "Viongozi wa dini msigeuze kuaminika na kuaminiwa kuwa fursa ya kutugawa na kuchochea chuki," baadhi ya waumini wenyewe wa kanisa hilo wameandika.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464