` UCHUMI WETU HAUNA LIKIZO YA MAANDAMANO: SAUTI ZA WAJASIRIAMALI ZINATAKA AMANI

UCHUMI WETU HAUNA LIKIZO YA MAANDAMANO: SAUTI ZA WAJASIRIAMALI ZINATAKA AMANI


Wakati Watanzania wakiendelea na shughuli zao za kujenga Taifa, wito wowote wa kufanya maandamano yasiyo na ukomo, kama ule unaotangazwa kwa Desemba 9, unazua hofu kubwa kwa jamii ya wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo. Wanaeleza wazi kuwa amani ni mtaji mkuu wa kiuchumi.

Kulwa Mtebe, mjasiriamali kutoka Bariadi, Simiyu, anasema wazi: "Suala la amani na utulivu katika nchi yetu ni la muhimu sana. Kwenye nchi tukikosa hivyo vitu, mambo ndiyo yanakuwa magumu zaidi. Biashara inategemea utulivu. Mauzo ya leo yanategemea amani ya jana." anasema Mtebe.

Aidha amesema katika mahojiano kwamba maandamano ya siku moja tu yanaweza kuingiza hasara ya mamilioni na kuvuruga minyororo ya ugavi, hasa kwa wajasiriamali wadogo wanaoishi kwa kipato cha siku. 

"Kama nchi ikikosa amani, hakuna jambo litafanyika, tunawaona wenzetu ukosefu wa amani unavyowatesa." alisema Mtebe

Wataalamu wa uchumi wanaonya kuwa mbali na hasara ya moja kwa moja, miito ya vurugu inapunguza imani ya wawekezaji wa ndani na nje. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza juu ya umuhimu wa kuwavutia wawekezaji; kauli hizi za maandamano zinahatarisha juhudi hizo.

Ujumbe mkuu kwa vijana na wajasiriamali ni kuepuka kurubuniwa na miito ya kutatiza shughuli za kiuchumi, kwani kufanya hivyo ni kujipiga pigo wenyewe. Amani ndiyo mwavuli unaolinda kazi, mitaji, na soko lao.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464