` BARAZA LA MADIWANI HALMASHAURI YA WILAYA YA KISHAPU LAZINDULIWA RASMI

BARAZA LA MADIWANI HALMASHAURI YA WILAYA YA KISHAPU LAZINDULIWA RASMI

 

NA EUNICE KANUMBA –SHINYANGA

Baraza la madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Kishapu   limezinduliwa rasmi tayari kwa kuanza utekelezaji  wa majukumu yake katika kipindi cha 2025/2030 huku diwani  wa kata ya Ndoleleji  Emanuel Limbe akichaguliwa kwa kura zote na baraza hilo kuwa mwenyekiti wa Halmashauri hiyo huku diwani wa kata ya Masanga Enock Bundala akichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Halmashauri.

Akizungumza katika kikao Desemba 3,2025 ambacho ni kikao cha kwanza  cha baraza la madiwani baada ya uchanguzi mkuu uliofanyika tarehe 29 october kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Kishapu Mkuu wa wilaya ya Kishapu ,Peter Masindi amewataka madiwani hao kuvunja makundi kwani uchaguzi ushaisha na badala yake wakasikilize na kutatua kero za wananchi.

Amesema wananchi wana imani na madiwani hao ndo maana waliwachagua ili wakawatumikie hivyo wanatakiwa kuwafikia wananchi kwa haraka katika maeneo yao na kutatua changamoto zao kwa wakati na pamoja na kujiepusha na maslahi binafsi katika miradi mbalimbali ya serikali itakayoletwa katika kata zao.

DC Masindi amewataka pia madiwani hao walioapishwa rasmi kuanza kazi kwenda kumaliza tofauti za kisiasa udini na ukabila katika maeneo yao pamoja na kuwalinda na kushirikiana na watumishi waserikali pasipo kuleta migogoro baina yao ili utekelezaji wa majukumu ya kuwadumia wananchi utekelezeke kwa weledi na kwa ufanisi.  

“Nendeni  mkakutane na wananchi waliowapa kura lakini pia mkahakikishe miradi ya maendeleo inaenda kwa wananchi na inatekelezeka kwa wakati”amesema DC Masindi

Kwa upande, Mwenyekiti wa Halmashuri hiyo Josephat Limbe ,akitoa neno la shukrani baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Halmashuri hiyo amesema wananchi katika wilaya ya Kishapu wanaitaji maendeleo pamoja hivyo atashirikiana nao kwa dhati na viongozi na wataalamu katika halmashuri  kuhakikisha kila kinatekelezeka kwa weledi.

Limbe amesema Wilaya ya Kishapu ina kata 29 vijiji 117 na vitongoji 660 hivyo ni eneo kubwa kijiografia lenye kuhitaji utulivu wa hali ya juu katika kutekeleza miradi ya maendeleo hivyo madiwani wakatekeleze hasa yale waliyohaidi katika kipindi cha kampeni  

 “Mimi binafsi ninaamini katika mashirikiano hivyo twendeni tukashirikiane na wananchi lakini tukasimamie   maelekezo ya Mheshimiwa Rais na yale tutakayokuwa tumekubaliana katika baraza letu ” amesema Limbe.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Emmanuel Johnson, amewataka madiwani hao hususani wale ambao ndiyo wameingia kwa mara ya kwanza katika baraza hilo  kusoma kanuni na miongozo ya baraza la madiwani ili kutekeleza majukumu yao kwa mujibu  kwa uadilifu na uwazi.

Shinyanga press club blog, Pia imeafanikiwa kuzungumza na baadhi ya madiwani  waliopishwa kwa kuanza majukumu yao akiwemo diwani wa kata ya Bubiki James Kasomi, ambapo amesema wananchi wamekuwa na matarajio makubwa mno na madiwani hao hivyo wanakwenda kurejesha matumani kwa kushughulikia miradi ya barabara ,zahanati pamoja na changamoto nyingine.

Lakini pia diwani wa viti maalumu kutoka kata ya Ukenyenge Sophia Julius Masele  ,amesema mara tu baada ya kuapishwa wanawahaidi wananchi kutimiza yale yote waliyohaidi katika kipindi cha kampeni kupitia kamati za kisekta na za kudumu za baraza la madiwani walizounda hivyo kwa ushirikiano wa pamoja wilaya ya Kishapu itasonga mbele.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464