
Kauli hii inatolewa huku Wito wa Kitaifa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kulinda amani ukiendelea kusambaa kwa kasi miongoni mwa wananchi na vijana.
Mchungaji Lusekelo ameeleza kuwa tukio hilo limekuwa uzoefu mchungu ambao Watanzania hawakuwahi kuupitia, akifananisha hali iliyotokea Oktoba 29 na "vita ya wenyewe kwa wenyewe," na kulifananisha na mazingira ya vita ya 1977/1978 dhidi ya Idd Amin.
Akitoa pole kwa wakazi wa Dar es Salaam, Arusha, Songwe na Mwanza walioathirika, amesisitiza kuwa hali hiyo iligusa Watanzania bila ubaguzi, akitaja hata baadhi ya waumini wake maeneo ya Kimara waliathirika.
Alisema ipo haja viongozi wa dini, wazazi, viongozi wa serikali na kisiasa kutafakari namna heshima ya nchi ilivyotikisika na umuhimu wa kurejea kwenye misingi ya umoja na ustaarabu.
Amewaonya Watanzania kuwa ni muhimu yale yaliyotokea yakawa funzo, kwani huenda Taifa likakumbana na tukio kubwa zaidi baada ya miaka michache ijayo endapo amani haitalindwa.
Maoni haya ya viongozi wa dini yanaungana na msimamo thabiti wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alitoa wito kwa Watanzania wote kulinda amani.
"Serikali Haitaruhusu Nchi Ivurugwe: Tutailinda Nchi kwa Nguvu Zote."
Wito huu umeelekezwa hasa kwa vijana, kuwakumbusha kuwa Amani ndiyo mtaji mkuu wa elimu, ajira, na biashara yao. Wamehimizwa kukataa kauli yoyote yenye nia ya kutugawa au kuvuruga utulivu tulionao.
Kauli za wananchi zilizotolewa mtandaoni baada ya tukio zinaonesha jinsi ujumbe huu unavyopokewa:Kujifunza na Kusamehe: Raia wengi wanakubaliana kwamba, "Ni kuelewana tu, tukikaa chini kila kitu kitakuwa sawa," huku wakisisitiza: "Tujitolee kusamehe, lakini tusisahau umuhimu wa kujifunza kutoka kwa makosa ya zamani."
Wananchi wamehimiza kuwa amani lazima idumishwe, lakini iambatane na haki kwa kila Mtanzania.
Ujumbe wa Rais umeeleza wazi kuwa kulinda nchi si kazi ya vyombo vya ulinzi pekee: "Ni jukumu la kila mmoja wetu, tukiwa na uzalendo na upendo kwa Taifa letu. Tuwe walinzi wa Amani katika familia, vitongoji, na maeneo yetu ya kazi."
Watanzania kwa ujumla wanakubaliana kwamba tukio la Oktoba 29 ni "kidonda tusichopaswa kuingiza tena mdudu", na kwamba suluhisho la kudumu linaanzia kwenye umoja, upendo na mazungumzo ya kiungwana.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464