
Sheikh wa Mkoa wa Mtwara, Sheikh Jamaldin Chamwi, ametoa wito mzito kwa viongozi, wanasiasa, wananchi, na wadau wote wa Taifa kuhakikisha wanakataa kuruhusu dosari zozote zinazoweza kutia doa amani na taswira ya Taifa la Tanzania.
Sheikh Chamwi alitoa wito huo hivi karibuni alipozungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari mkoani humo, katika ofisi ya Jumuiya ya Waislamu (BAKWATA) iliyopo Manispaa ya Mtwara Mikindani. Lengo kuu la wito wake lilikuwa kuwaomba Watanzania waendelee kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa kila mmoja kufuata mifumo na taratibu zilizowekwa kisheria ili kuepusha uvunjifu wa amani, akibainisha kuwa kwa miaka yote Tanzania imejipambanua kwa kuishi kwa amani. Hali hii imeifanya nchi kuwa kivutio kikubwa kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali.
“Wakazi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla ni vema kujiepusha na kiashiria chochote cha uvunjifu wa amani kwa Nchi kwani ikikosekana amani mambo mengi hayawezi kwenda,” alisema Sheikh Chamwi, akionya kuwa amani ndio msingi mkuu wa ustawi wa kiuchumi na kijamii.
Kwa upande mwingine, kauli ya Sheikh Chamwi imekuja wakati ambapo taarifa rasmi za Serikali zinasisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi na usalama.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anasema "Serikali Haitaruhusu Nchi Ivurugwe: Tutailinda Nchi kwa Nguvu Zote." .
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464