
Serikali ya Tanzania imemfungulia rasmi mashtaka ya uhujumu uchumi , Mange Kimambi,Mtanzania anayeishi nchini Marekani.
Taarifa kutoka kwenye tovuti rasmi ya Mahakama nchini Tanzania zinaonyesha kuwa kesi hiyo imepangwa kutajwa kwa mara ya kwanza Alhamisi wiki hii, Desemba 4 na ipo mbele ya Hassan Makube.
Hatua hii ya Serikali inakuja takriban mwezi mmoja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Hamza Johari, kumlaumu waziwazi mwanaharakati huyo. Bw. Johari alimtuhumu kuchochea vurugu zilizotokea katika siku ya uchaguzi uliopita.
Asubuhi ya Desemba 2, 2025, Mange Kimambi mwenyewe alionekana katika video fupi , akielezea kupokea taarifa za mashtaka hayo akisema anajiandaa.
Jana Rais Samia Suluhu Hassan amesema waliohamasisha vurugu siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu na siku zilizofuata walipanga kuangusha Dola, lakini serikali imeapa kuilinda nchi.
“Tunaapa kuilinda nchi hii na mipaka yake, kulinda usalama wa raia na mali zao, na katika hali hiyo nguvu inayotumika inaendana na tukio lililopo. Tunapoambiwa kwamba tulitumia nguvu kubwa sana kwenye tukio lile, nguvu ndogo ilikuwa ni ipi,” Rais Samia alihoji mbele ya wazee hao na viongozi wa serikali.
Aliongeza: “Kuna mengine nasikia yanapangwa, lakini Inshallah Mola hatosimama nao…litapeperuka.
“Lakini nataka niseme nilimsikia mmoja kati ya waandaaji wa nje anasema tarehe 9 (siku waliyopanga maandamano) iahirishwe isubiriwe siku ya Krisimasi sababu sasa hivi tumejipanga…nataka niwaambie wakati wowote wakija tumejipanga”.
Alisema lililotokea ni tukio la kutengenezwa na waliolitengeneza walidhamiria kuangusha Dola
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464