.jpeg)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza msimamo thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita kulinda amani, umoja na utulivu wa Taifa, huku akionya dhidi ya matamko yanayoashiria uchochezi.
Akizungumza kwenye mkutano maalum na Wazee wa Dar es Salaam, Rais Samia alitoa kauli kali akijibu mfululizo wa matamko yanayotolewa na baadhi ya taasisi za kidini, hususan Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
“Tupo tayari kukaa, kuzungumza na kuondoa mapungufu yaliyopo, lakini Serikali hii si ya kuamrishwa wala kupewa maelekezo,” alisema Dkt. Samia.
Rais Samia alifichua kuwa tangu aingie madarakani, TEC imetoa matamko takribani nane. Hata hivyo, alibainisha kuwa ndani ya Kanisa Katoliki lenyewe kuna tofauti za kimtazamo kuhusu uhalali na malengo ya baadhi ya kauli hizo.
Alisema baadhi ya viongozi na waumini wa Kanisa wanahoji kuwa matamko hayo hayajengwi katika misingi ya haki na ukweli, na hivyo kuchochea migawanyiko isiyo ya lazima katika jamii.
Rais alisisitiza kuwa Serikali haitavumilia kauli zozote zinazoashiria uchochezi ama zinazoweza kuvuruga misingi imara ya Taifa.
“Tanzania yetu ni nchi ya umoja, mshikamano, amani na utulivu, na hizo ndizo ngao zetu. Tusivurugwe ndugu zangu kupitia mirengo ya dini, siasa au mingineyo,” alihimiza Rais Samia.
Dkt. Samia alieleza masikitiko yake kuwa tuhuma dhidi ya Serikali ya Awamu ya Sita mara nyingi zimekosa msingi, akitaja mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali.
Aliuliza, "Kosa la Serikali ya awamu ya sita ni nini? Kueneza huduma bora za afya? Kupeleka elimu bora hadi vijijini? Kukuza uchumi hadi kutambuliwa duniani? Kuiweka Tanzania salama? Kosa letu ni lipi?"
Alisisitiza kuwa misingi ya kidemokrasia inaruhusu kukosoa, lakini sio kuhatarisha utulivu wa nchi.
Alitoa wito kwa wananchi kuvumilia na kutokubali vurugu kwa sababu za tofauti za kidini, asili, au mtazamo binafsi kuhusu kiongozi.
“Kama humpendi anayeongoza, stahimili. Mioyo yetu imeundwa kwa stahimilivu. Demokrasia ipo, ataongoza na ataondoka. Hakuna sababu ya kuvuruga nchi,” aliongeza.
Rais Samia alitoa wito mkali kwa viongozi wa dini kutojificha nyuma ya majoho na kujaribu kuongoza nchi.
Alisema, Tanzania itaendelea kuongozwa kwa mujibu wa Katiba na sheria, si kwa hisia ama matamanio ya mtu binafsi.
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu, lakini inatarajia taasisi za dini kubaki kuwa chachu ya maadili na sio jukwaa la mijadala inayoweza kupandikiza migawanyiko.
Rais aliwahimiza wananchi kutumia busara dhidi ya misimamo mikali na "sumu" wanayopewa, akibainisha kuwa dini mara nyingi hutumiwa kuwashawishi watu bila uchambuzi wa kina.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464