
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka bayana msimamo wa Serikali kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, akisisitiza kuwa suala hilo halipaswi kufanywa kwa shinikizo bali kwa njia ya maridhiano ya kitaifa.
Akizungumza hivi karibuni, Rais Samia alieleza kuwa ingawa Serikali inatambua umuhimu wa Katiba Mpya, mchakato wake ni wa hatua kwa hatua na unahitaji umoja wa wadau wote.
“Suala la Katiba Mpya ni mchakato unaotanguliwa na maridhiano…” — Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia alieleza kuwa Kabla ya kuanza rasmi kwa mchakato huo, ni muhimu kwa pande zote zinazovutana, zikiwemo Serikali, vyama vya siasa, na wadau wengine wa jamii, kukaa pamoja na kufikia maelewano ya msingi kuhusu mwelekeo wa Taifa.
Amesisitiza kuwa maridhiano hayo ndiyo nguzo pekee itakayohakikisha Katiba inayopatikana inakubaliwa na kila Mtanzania na inalinda maslahi mapana ya Taifa, badala ya kutumika kutimiza matakwa ya kundi au chama kimoja.
Aidha alisisitiza kwamba taifa haliwezi kwenda huko likiwa na maumivu ndio maana ameteua tume kuchunguza undani wa tukio na kuipa miezi mitatu, kisha taarifa hizo ziende kwa wadau kufikia maridhiano na ndipo mchakato wa katiba uanze.
Aidha alisema katika kuendesha nchi hakuna maelekezo ya masharti ya mazungumzo na kufikia maridhiano kutoka pande zozote zikiwamo taasisi za kidini.
“Kikatiba na sheria za nchi hakuna madhehebu hata moja ya dini yoyote imepewa uwezo kikatiba na kisheria kutoa matamko yaku-overide madhehebu mengine yote ya dini, hakuna. Viongozi wa dini msijivishe majoho ya kwamba ninyi ndio mnaweza ku-overun nchi hii, hakuna, hakuna. Tutakwenda kwa Katiba na sheria ya nchi hii, hatutaendeshwa na madhehebu yoyote ya dini,” alisema Rais Samia.
Aliongeza: “Hakuna kitabu chochote cha dini kimesema tutazitumia dini zetu kuvuruga nchi zetu, hakuna. Ni utashi binafsi wa watu kwa ubaya wa nafsi zao. Kwa hiyo msivae majoho ya dini mkatengeneza utashi wenu binafsi kwa kupitia vivuli vya dini”.
Alisema ingawa Watanzania wana dini, lakini nchi haina dini na hakuna dhehebu lolote yenye mamlaka ya kipekee ya kutoa matamko yanayojipa nguvu au mamlaka juu ya dhehebu jingine.
Alibainisha kuwa hakuna mtu aliyepewa cheti cha kusema nchi ni yake au kuamua namna nchi itaendeshwa, na kufafanua kuwa Tanzania itaendelea kuongozwa kwa misingi ya demokrasia iliyokubaliwa na wote.
Amewataka viongozi wa dini wasijivike joho la kuwa na nguvu ya kuitawala nchi kwa sababu nchi inatawaliwa na Katiba na sheria na kuwa haitaendeshwa kwa misingi ya madhehebu ya dini.
Amekosoa tabia ya baadhi ya watu kuitumia dini kama kisingizio cha chuki dhidi ya viongozi, akisema hatua hiyo ni hatari kwa taifa, akihoji kosa la serikali ni lipi kwa sababu kama ni uchumi umekua, na mafanikio ni mengi yameletwa na serikali.
Alionya sumu inayopandikizwa kupitia dini kwa lengo la kumchafua mtu, akieleza kuwa chuki ya kidini huacha alama ya kudumu moyoni kuliko propaganda za kisiasa.
“Wanasiasa wakimharibu mtu, wanamharibu kichwani. Kichwa kinakubali akija mwanasiasa mwingine anasema lililo jema kichwa kinafuta lile baya na kukubali hilo zuri, lakini ukimharibu mtu kwenye dini, chuki inaingia moyoni na ikishaingia ni hatari zaidi,” alieleza Rais Samia.
Hivyo aliwataka viongozi wa dini kukaa kwenye mstari wao wa kiroho, na kuonesha sura halisi ya majoho yao na kutotumia kivuli cha dini kwa maslahi binafsi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464