` DCEA YAVUNJA MTANDAO WA DAWA ZA KULEVYA—MALI ZA BILIONI 3.3 ZATAIFISHWA

DCEA YAVUNJA MTANDAO WA DAWA ZA KULEVYA—MALI ZA BILIONI 3.3 ZATAIFISHWA

  

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikisha ukamataji wa jumla ya kilogramu 3,799.22 za dawa za kulevya, kuteketeza ekari 18 za mashamba ya bangi pamoja na kutaifisha mali za wahalifu zenye thamani ya shilingi bilioni tatu na milioni mia tatu na nne (3,304,000,000/=) katika operesheni mbalimbali zilizofanyika mwezi Novemba. Jumla ya watuhumiwa 84 walikamatwa kuhusiana na uhalifu huo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali Lyimo alisema kuwa, katika kuendeleza jitihada za kukabiliana na uhalifu wa dawa za kulevya, Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ilitoa amri ya kutaifishwa kwa mali za watuhumiwa Saleh Khamis Basleman na Gawar Bachi Fakir, zenye thamani ya shilingi Bilioni tatu na milioni mia tatu na nne (3,304,000,000/=), baada ya kuthibitika kuwa wanahusika na biashara ya dawa za kulevya. Mali hizo ni pamoja na nyumba, viwanja na magari.

Amesema maombi ya kutaifishwa kwa mali hizo yaliwasilishwa mahakamani kufuatia uchunguzi ulioonyesha kuwa watuhumiwa walimiliki mali zilizopatikana kupitia biashara haramu ya dawa za kulevya. Utaifishaji huo umefanyika kwa mujibu wa Sheria ya Mazao ya Uhalifu Sura ya 256 ikisomwa pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa Sura ya 200, sambamba na Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015.

“Utaifishaji wa mazalia ya uhalifu umewekwa kisheria ili kuifundisha jamii kuwa uhalifu hauna faida. Adhabu za kifungo pekee hazitoshi kutokomeza uhalifu, hususan ule unaopangwa kama makosa yanayohusiana na dawa za kulevya. Huu ni mkakati wa kuzuia uhalifu kuendelea na kuondoa matamanio ya kufanya uhalifu,” alisema Kamishna Jenerali Lyimo.
Amezitaja mali zilizotaifishwa kuwa ni apartment namba OA2 ghorofa ya kwanza katika Sea Breeze Residential Complex, kiwanja namba 192 block “O” Jangwani Beach; apartment 6B katika kiwanja namba 26 block 52 Kariakoo; nyumba katika viwanja namba 329 na 1009 block “C” Mbezi; kiwanja namba 69 block 7 Mbweni JKT; nyumba namba 14 kiwanja namba 131 block 9 Mtoni Kijichi; na kiwanja namba 44768 Kigogo, Kisarawe II, Kigamboni. Pia kiwanja kilichopo Shungubweni Village wilayani Mkuranga.

Mali nyingine ni kiwanja namba 53 block E Boza Village Mkuranga; kiwanja kingine kilichopo Boza Village; kiwanja namba 8 block C Mwambao, Bagamoyo; apartment namba PA1 ghorofa ya chini Sea Breeze Residential Complex, kiwanja namba 192 block P; nyumba namba 9 Magomeni, Ubungo; pamoja na viwanja namba 44746, 44748 na 44789 vilivyopo Kigogo, Kisarawe II, Kigamboni.

Ametaja pia magari yaliyotaifishwa kuwa ni T 539 DKQ (Nissan Civilian), T 427 EAH (Subaru Impreza), T 196 EAC (Volkswagen), T 654 DCH (Volkswagen), T 141 DKV (Nissan Civilian), T 944 DKY (Nissan Civilian), T 830 DLA (Nissan Civilian), T 767 DLL (Nissan Civilian), T 435 DJY (Toyota Corolla Spacio), T 307 DLW (Nissan Civilian) na T 753 DKS (Nissan Civilian).

Kadhalika, katika operesheni zilizofanyika jijini Dar es Salaam, watuhumiwa Cuthbert Kalokola (34) na Murath Abdallah (19) walikamatwa Sinza D wakiwa na vidonge 738 vya dawa mpya aina ya 3,4 - Methylenedioxymethamphetamine (MDMA) vyenye uzito wa gramu 177.78, pamoja na vidonge 24 vya dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Rohypnol vyenye uzito wa gramu 10.03.

Katika eneo la Mbezi Maramba Mawili, watuhumiwa saba Jaribu Tindwa (38), Ally Meshe (39), Juma Mfamo (20), Rahim Nampanda (28), Abubakari Ally (20), Nurdin Rashid (36) na Farid Rashid (33) walikamatwa wakiwa na kilogramu 90 za dawa za kulevya aina ya skanka zilizokuwa zimefichwa ndani ya matanki ya zilizofichwa ndani ya matanki ya solar panel yaliyopakiwa kwenye basi la Falcon aina ya Scania lenye namba za usajili T372 DFK linalosafiri kati ya Tanzania na Malawi.

Vilevile, katika mpaka wa Kasesya mkoani Rukwa, Godwin Andrew (26) mkazi wa Mbalizi Mbeya alikamatwa akiwa na kilogramu 244.3 za skanka zilizofichwa ndani ya spika, mashine za kupooza hewa, mashine za kukatia majani na vifaa vya kompyuta (CPU). Mzigo huo ulikuwa unasafirishwa kwa gari aina ya Iveco Van lenye namba za usajili za nchi ya Afrika Kusini CN 85 FN GP mali ya kampuni ya Makamua Logistics Limited.

Aidha, katika operesheni nyingine zilizofanyika mikoa mbalimbali, zilikamatwa kilogramu 2,041.45 za bangi, kilogramu 1,423.28 za mirungi, na ekari 18 za mashamba ya bangi ziliteketezwa. Magari manne na pikipiki 12 pia vilikamatwa. Akitoa ufafanuzi kuhusu operesheni hizo, Kamishna Jenerali Lyimo alisema kuwa hatua zilizochukuliwa jijini Dar es Salaam ni sehemu ya utekelezaji wa udhibiti wa tatizo la dawa za kulevya nchi nzima.

“Operesheni hizi zinafanyika maeneo yote nchini ili kuzuia uhalifu wa dawa za kulevya na kufuta kabisa mtandao wa dawa hizo” amesisitiza Lyimo.

DCEA imetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka hiyo kwa kutoa taarifa za uhalifu wa dawa za kulevya ili kufanikisha mapambano dhidi ya janga hilo.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464