` MITANDAONI MOTO WAWAKA BAADA YA SERIKALI KUTAJA MIPANGO YA VURUGU INAYODAIWA KUFADHILIWA NA NJE

MITANDAONI MOTO WAWAKA BAADA YA SERIKALI KUTAJA MIPANGO YA VURUGU INAYODAIWA KUFADHILIWA NA NJE


Kauli ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, kwamba kiasi cha Dola za Marekani milioni mbili (sawa na takribani Shilingi Bilioni 4.5) zimetolewa kwa ajili ya kuchochea chokochoko na vurugu nchini, limezua mjadala mkali mtandaoni. 

Watumiaji wa mitandao ya kijamii wamejikita katika kuchambua chanzo cha vurugu, maslahi ya mataifa ya kigeni, na umuhimu wa busara katika kushughulikia masuala ya kitaifa.

Waziri Mkuu alisema kuwa wachochezi wamelenga kuharibu uchumi wa nchi na kurudisha nyuma maendeleo, huku lengo kuu likiwa ni kunyakua rasilimali adimu za Tanzania kama vile madini ya Uranium na maendeleo ya miradi ya gesi asilia.

Baada ya ufichuzi huo, maoni yamegawanyika kati ya wale wanaosisitiza umuhimu wa kufahamu maslahi ya Taifa na wale wanaotilia mkazo umakini wa vijana kujitambua.

Mchangiaji Oliver Kibua alikaribisha ufichuzi wa Serikali, akisisitiza umuhimu wa wananchi kujua chanzo na sababu ya vurugu hizo:"Afadhali kama inaweza kuwaambia wananchi sababu na chanzo cha yote wajue kipindi watu wanatumika na kuhadaika kuwa wapiganie haki kumbe wenzao wana wanachokitaka, na vurugu ikiwepo waumiao ni wananchi waliopo nchini na sio nje ya nchi."

Kibua pia alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kufahamu kuwa hakuna taifa linaloingilia kati masuala ya nchi nyingine bila maslahi yao binafsi. Alihimiza, "Hao wanaojitambua waamke maana wanajitambua wao hawatambui ukweli wa mambo... think before you act."

Mchangiaji mwingine alitumia nafasi hiyo kukosoa matumizi ya lugha ya matusi na mihemko katika mijadala ya kitaifa, hasa kwa wale waliowahi kushika nyadhifa za uongozi.

"...Nikuona watu waliowahi kuwa madarakani mahali fulani wakakosana na waliowaweka madarakani wanavyokuwa hawajui kutumia lugha ya ushawishi na badala yake wanatukana... Si suala tu la kuamsha hisia bali ni suala la kusoma, kutafakari na kuona kweli katika muda sahihi na mazingira sahihi." alisema mmoja wa wachangiaji hao.

Mchangiaji huyo alitumia fumbo la kijadi kuhusu njiwa waliokosa ushauri na kufa ufukweni, akisisitiza kuwa nguvu (mihemko) bila maarifa (busara na ushauri) haisaidii. Alihimiza Watanzania kuchanganya maarifa ya kimagharibi na hekima za zamani ili kupata majibu sahihi.

Hata hivyo Rafael Valency Kwembe alionyesha imani kwa vijana wa Afrika, akisema:"Uzuri waafrika wa sasa tunajitambua sana, nyie pigeni ngonjera ila ukweli tunaujua na tunaufanyia kazi. Tunajua nani anazingua na nani yupo sahihi."

Mchangiaji mwingine aliunga mkono msimamo wa Serikali kwamba vurugu hizo zinaletwa na wanaharakati wanaolipwa na kuwahimiza Watanzania kuamka na kuchukua tahadhari, akisisitiza: "Ajira na uondoaji wa umaskini utapatikana tu nchi ikiwa na amani."

Kauli ya Waziri Mkuu inahimiza Watanzania kujiuliza maswali kuhusu maslahi na ajenda ya watu wanaotoa malipo hayo. Alionya kuwa mbinu hizi zimetumika katika nchi zingine barani Afrika, ambapo chokochoko huanzishwa ili kuruhusu uvurugaji na uchukuaji wa rasilimali, kabla ya wachochezi kuondoka baada ya rasilimali kuisha.

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464