hali ya wasiwasi inayoendelea nchini, hasa kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa vurugu zingine, kuanzia Desemba 9 sauti ya wazazi na wafanyabiashara wadogo inazidi kupaaa ikihimiza watoto wao waepuke vurugu, wakisisitiza kwamba maisha yao yanategemea amani na utulivu.
Mama Zawadi, mchuuzi mzoefu wa soko la Kariakoo, amekuwa kinara wa kuakisi hofu ya Watanzania ambao maisha yao huhesabiwa kwa faida ya siku.
Akizungumza kwa hisia, Mama Zawadi alieleza: “Mimi ni Mama Zawadi, mchuuzi wa soko la Kariakoo, na naongea kwa niaba ya maelfu ya Watanzania ambao maisha yetu hutegemea kupata riziki ya kila siku. Ninaposikia wito wa maandamano yenye vurugu, moyo wangu unajawa na hofu isiyoelezeka.”
Woga wake mkubwa unahusu jinsi ghasia zinavyokwamisha shughuli za kiuchumi. "Maandamano yanamaanisha masoko kufungwa, biashara kusimama, na uwezekano wa kupoteza kipato ambacho ndio mlo wa watoto wetu," alifafanua.
Alitoa onyo kali kwa vijana: "Tunaweza vipi kupata chakula kama hatuwezi kufanya kazi? Kusimamisha nchi ni sawa na kutuhukumu kifo kwa njaa.”
Aidha, Mama Zawadi aliweka bayana athari za machafuko kwa kundi la wagonjwa sugu, kama wa UKIMWI na Kisukari, ambao maisha yao yanategemea upatikanaji wa huduma za afya bila kukosa.
Alisimulia maelezo ya mmoja wa wagonjwa alisema, "Kukiwa na machafuko, hospitali zinasita kufanya kazi, usafiri unakwama. Tutapata wapi dawa zetu? Bila dawa, afya yetu inazidi kuzorota. Tunaomba huruma!’”
Mama Zawadi alimalizia kwa kuwataka vijana kutafuta suluhu kupitia mazungumzo na kuonya: "Kuna ndugu zetu tayari wamepoteza wapendwa wao... maandamano yenye ghasia yataacha majonzi ya kudumu."