
Serikali imefichua kuwa chokochoko na vurugu zinazoendelea nchini zimeletwa na wanaharakati wanaolipwa kwa lengo la kuharibu uchumi wa nchi na kurudisha nyuma maendeleo.
Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kukataa kushawishiwa na wanaharakati hao.Waziri Mkuu ameeleza kuwa baadhi ya vijana walio nje ya nchi wamebainika kupokea kiasi cha Dola za Marekani milioni mbili (sawa na takribani shilingi bilioni 4.5) ili kuchochea vurugu nchini. Alihimiza watanzania kujiuliza maswali kuhusu maslahi na ajenda ya watu wanaotoa malipo hayo kwa nchi.
Kulingana na maelezo ya Waziri Mkuu, lengo kuu la wachochezi hawa ni kunyakua rasilimali adimu za Tanzania. Alitaja ugunduzi wa Uranium (Tanzania ikiwa nchi ya tisa duniani na ya kwanza Afrika kwa tani za ujazo 890,000) na maendeleo ya miradi ya gesi asilia kama vivutio vikubwa vinavyowafanya waivuruge Tanzania.
"Hawa watu wanalenga tugombane ili wachukue madini adimu (rare earth minerals)... Wanajua Tanzania ina gesi asilia nyingi na inakaribia kuanza," alionya Waziri Mkuu.
Amesisitiza kuwa mbinu hizi zimetumika katika nchi zingine barani Afrika, ambapo chokochoko huanzishwa ili kuruhusu uvurugaji na uchukuaji wa rasilimali, kabla ya wachochezi kuondoka baada ya rasilimali kuisha.
Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania "kuamka na kuchukua tahadhari" dhidi ya mchezo huu, akisisitiza kuwa ajira na uondoaji wa umaskini utapatikana tu nchi ikiwa na amani.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464