
Kampeni kubwa ya kukataa maandamano yanayolenga kuvuruga amani na utulivu wa nchi imechukua kasi, huku sauti za vijana, hasa mabinti, zikiibuka kwa nguvu kupinga vitendo hivyo. Wakizungumza kwa umoja, wametoa wito kwa vijana wenzao kuacha kutumiwa na watu wenye maslahi binafsi na badala yake waendelee kulinda amani waliyozaliwa nayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Alhamisi Disemba 4, 2025, Bi. Beatrice Mwahegili, Katibu Msaidizi wa idara ya Mabinti na Uwezeshaji wa Taasisi ya Mama Asemewe, alisisitiza kuwa hakuna Tanzania nyingine na gharama ya kurejesha amani pale itakapopotea ni kubwa mno.
"Tunapinga vikali maandamano yanayoendelea kuhamasishwa tarehe 09. Tarehe tisa ni siku ambayo Taifa letu lilipata uhuru, si siku ya vurugu au kuhamasisha machafuko katika Tanzania yetu," alisema Bi. Beatrice huku akisisitiza wajibu wa kwanza wa vijana kuitunza amani.
Ameongeza kwa kuwataka vijana "kuamka na kutokubali kutumika kwa maslahi ya watu wachache," na kuwakataa wale wote wanaohamasisha vitendo vya uvunjifu wa amani nchini.
Mwahegili alibainisha wazi kuwa amani iliyopo ndio msingi wa maendeleo na ustawi wa mabinti, vijana, na jamii nzima ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa fursa lukuki za kiuchumi.
"Kipindi cha Rais Samia ametugusa mabinti kwa asilimia kubwa sana," alisisitiza kiongozi huyo wa vijana, akieleza jinsi fursa hizi zinavyowapa vijana kipaumbele na kuwaondoa katika hatari ya kutumiwa kisiasa.
Katika muktadha huu, Kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa mwelekeo wa jinsi serikali ilivyojiandaa kukabiliana na changamoto zozote zinazoweza kutishia amani. Akihutubia taifa hivi karibuni, Rais Samia alisisitiza kuwa jukumu la kwanza la serikali ni kulinda usalama wa raia na mali zao.
Rais alieleza kuwa serikali ina mipango imara ya kuhakikisha utulivu unaendelea, akibainisha kuwa uhuru wa kukusanyika na kutoa maoni unapaswa kuheshimu sheria na kanuni zilizopo nchini.
"Hatutakubali mikakati yoyote ile itakayolenga kurudisha nyuma maendeleo yetu tuliyoyapata kwa jasho na damu. Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimeelekezwa kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria dhidi ya yeyote atakayejaribu kuvuruga amani yetu," alisema Rais Samia.
Kauli hiyo ya Rais inaakisi maandalizi ya serikali ya kisheria na kiulinzi, huku ikituma ujumbe wazi kwamba wakati serikali iko tayari kusikiliza maoni, haitavumilia vitendo vinavyohatarisha usalama wa Taifa.