Picha ya pamoja ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Emmanuel Johnso (wa nne kulia) na madereva wa Halmashauri hiyo katika kikao kazi maalum kilicholenga kuimarisha maadili ya kazi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Emmanuel Johnson amekutana na madereva wa Halmashauri hiyo katika kikao kazi maalum kilicholenga kuimarisha maadili ya kazi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akizungumza Disemba 19,2025 katika kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo,Mkurugenzi Johnson amesisitiza umuhimu wa madereva kuzingatia maadili ya kazi kuanzia kwenye matengenezo ya magari, matumizi sahihi ya rasilimali za Serikali pamoja na utunzaji wa vyombo vya usafiri wanavyovisimamia.
Ameeleza kuwa madereva wanapaswa kutambua nafasi yao muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya Halmashauri, kufanya kazi kwa kujiamini, uaminifu na kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya utumishi wa umma.
“Madereva ni sehemu muhimu ya mfumo wa utoaji huduma. Ni wajibu wenu kuhakikisha magari yanatunzwa vizuri, yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na mnafanya kazi kwa uadilifu na kujiamini,” amesema Mkurugenzi Johnson.
Aidha, amewataka madereva kuwa na tabia ya kueleza changamoto wanazokutana nazo kazini, ili uongozi uweze kuzifanyia kazi kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji ameielekeza Idara ya Utumishi kuhakikisha inakuwa na utaratibu wa kukutana na madereva wapya mara kwa mara, ili kuwakumbusha maadili ya kazi, haki na wajibu wao pamoja na kuboresha taratibu za ufanyaji kazi ndani ya Halmashauri.
Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu za kuimarisha nidhamu, uwajibikaji na ubora wa huduma kwa wananchi kupitia usimamizi mzuri wa rasilimali watu na mali za umma.