
Na Stella Herman,Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema Serikali haitakuwa tayari kumvumilia mtu yeyote anayekwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa maslahi binafsi, jambo linalosababisha wananchi kuchelewa kupata huduma ilhali fedha tayari zimetolewa.
Mhita ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na madiwani pamoja na wakuu wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, akisisitiza kuwa si jambo linalokubalika kwa wananchi kuendelea kukosa huduma baada ya changamoto zao kuwasilishwa na viongozi wao na Serikali kuchukua hatua ya kutoa fedha.
Amesema lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuwawezesha kuondokana na matatizo yao na kusonga mbele kimaendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano katika kuijenga Halmashauri ya Kishapu.
“Nendeni mkasimamie miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yenu ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi ambao ndio waliowapa dhamana ya kuwaongoza. Pale panapokuwa na changamoto, toeni taarifa kwa Mkurugenzi ili hatua zichukuliwe,” amesema Mhita.




Pia amewataka viongozi hao kuendelea kubuni na kusimamia vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani, jambo litakaloongeza mchango wa asilimia kumi unaotokana na mapato hayo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha, Mhita amesisitiza umuhimu wa kusimamia zao la pamba, ambalo ni tegemeo kubwa kwa wakulima na chanzo muhimu cha uchumi wa Halmashauri ya Kishapu.
“Mna dhamana kubwa ya kusimamia zao la pamba ili liendelee kuipa heshima Halmashauri yetu ya Kishapu. Hakuna sababu ya sisi kutosonga mbele, maana hili ni zao letu kubwa la biashara,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kishapu, Josephat Limbe, amesema viongozi wa Halmashauri hiyo watatekeleza kikamilifu maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa, ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha watumishi wazembe wanaokwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mamlaka husika, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati.




















