Meneja wa Afya na Usalama katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Dkt. Nicholas Mboya, akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Nyamongo, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwl. Saul Mwaisenye (katikati), akikagua moja ya mabanda ya huduma za afya na ushauri katika maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Nyamongo, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwl. Saul Mwaisenye, akikabidhi kadi ya Bima ya Afya kwa mmoja wa akina mama wazee wakati wa maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Nyamongo, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwl. Saul Mwaisenye, akikabidhi kadi ya Bima ya Afya kwa mmoja wa wazee wakati wa maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Nyamongo, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime
Wananchi wakipata ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya afya wakati wa maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Nyamongo, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Wazee wakiwa wamejipanga mstari kwa ajili ya kupokea kadi za Bima ya Afya kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wakati wa maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Nyamongo, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwl. Saul Mwaisenye (katikati mbele), akiongozwa kukagua mabanda ya huduma za afya na ushauri katika maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Nyamongo, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwl. Saul Mwaisenye, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na wafanyakazi wa Mgodi wa North Mara, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Kampuni ya RIN kwenye maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Nyamongo.
**
Katika dhamira yake ya kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha huduma katika sekta ya afya nchini, Mgodi wa Barrick North Mara uliopo wilayani Tarime mkoani Mara, umewezesha na kuungana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya na wadau wengine kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani mwaka huu wa 2025.
Maadhimisho ya mwaka huu yenye kauli mbiu isemayo “Shinda Vishawishi, Imarisha Mwitiko, Tokomeza UKIMWI” katika wilaya ya Tarime yamefanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari ya Igwe, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni , Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Tarime, Mwl. Sauli Mwaisenye aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowele.
Mwaisenye akiongea katika maadhimisho hayo alitoa wito kwa jamii kujali malezi na matunzo mazuri kwa watoto ambao wazazi wao wamefariki dunia kutokana na UKIMWI.“Watoto yatima ambao wamepoteza wazazi wao kutokana na janga la UKIMWI watunzwe na kupatiwa haki zao za msingi,”,alisisitiza.
Alisema serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali Serikali imeweka mkakati wa kubaini vyanzo vya maambukizi mapya na kupima VVU, pamoja na kuzingatia suala la tohara salama kwa wanaume, miongoni mwa hatua nyingine.
Taarifa zilizotolewa katika maadhimisho hayo zinaonesha kushuka kwa maambukizi ya VVU katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kutoka asilimia 1.5 mwaka 2024 hadi 1.42 kufikia Novemba 2025.
Aidha, halmashauri hiyo imetumia maadhimisho hayo kuwapatia wazee kadi za Bima ya Afya 2,000 ili kuwawezesha kupata huduma za matibabu kwa urahisi kwa ufadhili wa kampuni ya RIN ambayo ni moja ya wakandarasi wazawa wanaofanya biashara na mgodi wa Barrick North Mara.
Kwa upande wake Meneja wa Afya na Usalama katika Mgodi wa Barrick North Mara. Dkt. Nicholaus Mboya alisema suala la afya na usalama ni moja ya kipaumbele kikubwa kwa kampuni ya Barrick na ndio maana imekuwa ikishiriki kudhamini maadhimisho haya kwa ngazi ya wilaya kila mwaka pia imekuwa ikishirikiana na ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya kuwezesha wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na mgodi kupimwa afya zao na kupatiwa ushauri nasaha kuhusiana na mapambano ya UKIMWI na magonjwa mengine hatarishi kwenye jamii.
"Kama mgodi, tumejitolea kuwa majirani na washirika wema, tukisaidia jitihada za kuboresha maisha na kuimarisha afya ya jamii. Mchango wetu kwenye sekta ya afya ni muhimu sana pamoja na ushiriki kwenye kampeni mbalimbali za afya kama hizi za upimaji wa VVU na magonjwa mengineyo,” alisema Dkt. Nicholaus Mboya
Mbali na kuunga jitihada za kutokomeza UKIMWI na magonjwa mengineyo, Dk. Mboya alisema Barrick North Mara imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya afya kupitia fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ambayo inazidi kunufaisha jamii zinazoishi maeneo yanayozunguka mgodi.
Kwa mujibu wa Dkt. Mboya, Barrick imetumia takriban shilingi bilioni 5.4 sawa na asilimia 20 ya bajeti yake ya CSR katika mgodi wa North Mara kugharimia miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, nyumba za watumishi wa afya na ununuzi wa vifaa tiba tangu mwaka 2019 ilipochukua uendeshaji wa mgodi huo.
"Kwa mwaka huu wa 2025, kuna miradi ya afya ipatayo 21 yenye thamani ya Tsh. 2.4 bilioni ambayo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji na mingi ikiwa imekamilika,”alidokeza katika sehemu ya taarifa yake kwenye maadhimisho hayo.
Mbali na kupiga vita mambukizi ya VVU, wananchi waliohuduria maadhimisho hayo walisema yanasaidia kuhamasisha jamii kuepukana na vitendo vya ukatilii wa kijinsia, hususan kwa watoto na wanawake.
“Maadhimisho haya ni chachu ya maendeleo katika maeneo yetu yanayozunguka mgodi wa North Mara maana husadia watu kujua hali za afya zao,” alisema mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Getango Petro.
Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani hufanyika Desemba 1 kila mwaka kutathmini mwenendo wa hali ya VVU ili kuimarisha mikakati ya kuzuia mambukizi mapya na kuwakumbuka watu waliokufa kutokana na janga hilo, miongoni mwa mambo mengine.
Wakati huo huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi, alisema serikali itaendelea kuboresha huduma kwa wenye VVU, ikiwemo kuwapa dawa za ARV za kufubaza virusi hivyo bure.







