` ASKOFU ANGLIKANA ASISISTIZA MATUMIZI BORA YA MITANDAO , AMANI

ASKOFU ANGLIKANA ASISISTIZA MATUMIZI BORA YA MITANDAO , AMANI


Viongozi wa dini na watumishi wa Mungu nchini wamewataka Watanzania kuendelea kulinda amani, kutumia mitandao ya kijamii kwa faida chanya, na kupuuza miito yoyote ya kuandamana, hususan ile inayolenga tarehe 9 Desemba.

Akizungumza hivi karibuni, Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Morogoro, Godfrey Sehaba, alisisitiza umuhimu wa mitandao ya kijamii kama 'baraka' ambayo inaweza kutumika kuhubiri Injili, kutoa mafundisho, na kuiweka jamii katika maadili.

"MITANDAO ya kijamii ni baraka na inaweza kutusaidia Kanisa kuhubiri Injili, kutoa mafundisho na kuiweka jamii katika maadili," alisema Askofu Sehaba.

Hata hivyo, Askofu Sehaba alionya kuwa mitandao hiyo inaweza kuwa 'janga' kwa jamii endapo itatumika vibaya. "Nikiwa kiongozi wa dini ningeomba watu wote tunaotumia, tuitumie kuleta faida chanya kwa Watanzania," alisisitiza.

Kauli yake iliungwa mkono na Katekista wa Kanisa la Anglikana, Parishi ya Kisaki – Nyalutanga, Wilaya ya Morogoro, Joshua Msagala, ambaye alitilia mkazo uhusiano kati ya amani na injili ya wokovu.

"TUNAPOHUBIRI habari ya wokovu lazima amani iwepo na ndio maana hata ujio wa Yesu Kristo, jambo la kwanza kulikuwa na amani," alisema Katekista Msagala. "Sisi vijana wanakwaya tutajitahidi kutunga nyimbo zenye kuhamaisha amani."

Aidha, Mkurugenzi wa Hospitali ya Berega, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Mchungaji Canon Mgeya, alisisitiza umuhimu wa kuombea viongozi na kudumisha ulinzi wa amani ya nchi.

"Ni muhimu kwa wananchi kulinda amani ya nchi yetu na pia kuwaombea viongozi wa serikali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri Mkuu Dk Mwingulu Nchemba, mawaziri na viongozi wote wenye mamlaka katika nchi yetu ili kwa pamoja watuongoze katika haki na kweli," alihitimisha Mchungaji Canon Mgeya.

Viongozi hao wa dini wametoa wito kwa umma kupuuza taarifa za uchochezi na miito ya kuandamana iliyosambazwa kupitia mitandao ya kijamii inayolenga kufanya ghasia, hususan Desemba 9, na badala yake kuelekeza nguvu katika shughuli za maendeleo na matumizi mazuri ya teknolojia. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464