` SALUM KITUMBO MEYA MPYA WA MANISPAA YA SHINYANGA,PENDO SAWA NAIBU MEYA

SALUM KITUMBO MEYA MPYA WA MANISPAA YA SHINYANGA,PENDO SAWA NAIBU MEYA


Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, wamemchagua Diwani wa Kata ya Mjini, Salum Kitumbo kuwa Meya mpya wa Manispaa hiyo, huku Diwani wa Ndembezi Pendo Sawa, akichaguliwa kuwa Naibu Meya.

Uchaguzi huo umefanyika leo Desemba 4, 2025 katika kikao cha Baraza la Madiwani mara baada ya madiwani hao kuapishwa rasmi.
Msimamizi wa Uchaguzi huo ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga,Said Kitinga, amesema jumla ya wapiga kura ni 23, na kwamba wagombea wote wawili wamepigiwa kura za ndiyo 23 na hivyo kupata ushindi wa kishindo.

“Kwa mamlaka niliyopewa, natamka rasmi kwamba Salum Kitumbo ndiye Meya wa Manispaa ya Shinyanga na Pendo Sawa kuwa Naibu Meya,” amesema Kitinga.

Kitumbo akizungumza mara baada ya kuchaguliwa kuwa Meya wa Manispaa hiyo, amesisitiza kasi ya ukusanyaji wa mapato kutoka sh.bilioni 6.7 ambayo hukusanywa sasa hadi ifike sh.bilioni 10.

Aidha, amewataka Madiwani kufanya kazi kwa kushirikiana na Wataamu wa Halmashauri katika suala zima la ukusanyaji wa mapato pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo.

“Naombeni sana Madiwani na Wataalam wa Halmashauri tuongezeni kasi ya ukusanyaji wa mapato na tupunguze matumizi yasiyi ya lazima,”amesema Kitumbo.
Katika hatua nyingine ameagiza mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri kwamba inapokuwa ikitolewa iwafikie walengwa wote, pamoja na kusimamia urejeshwaji wa mikopo hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze, ameahidi ushirikiano wa kutosha kwa madiwani hao katika kusukuma gurudumu la maendeleo la Manispaa hiyo.

Mara baada ya uchaguzi huo, Baraza la Madiwani pia liliunda kamati mbalimbali za kudumu za Halmashauri kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Manispaa hiyo.

TAZAMA PICHA👇👇
Meya mpya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo akizungumza.
Meya mpya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo akizungumza.
Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Pendo Sawa akizungumza.
Meya mpya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo (kulia)akiwa na Naibu Meya Pendo Sawa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shuinyanga Alexius Kagunze akizungumza.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga Said Kitinga akitangaza matokeo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464