
Wakati Tanzania ikiendelea kufurahia utulivu wake wa kudumu, kauli za busara zimeendelea kutolewa na wazee wa Taifa pamoja na wadau mbalimbali, wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na kutoa onyo kali kwa vijana dhidi ya kutumiwa na makundi yenye nia ya kuvuruga nchi.
Wazee hao, wamechukua jukwaa la mijadala ya kijamii kueleza kwa hisia jinsi maisha yanavyoweza kuyumba ghafla endapo amani itatoweka, huku wakikumbusha historia ya uongozi wa nchi. Walieleza jinsi marais wote waliopita, kuanzia Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, walivyoiweka nchi katika misingi ya amani thabiti.
"Wazee wetu wametuongoza vizuri kuanzia Kambarage, ametoka Kambarage akaingia mzee Mwingi (Ali Hassan Mwinyi)... yaani marais wote waliopita hapa walituongoza kwa amani," alisema mmoja wa wazee, Ally Bomba Omary akionyesha masikitiko yake. Aliongeza, "Matatizo haya yametokea wapi hata haieleweki? Watu hawa wametokea wapi? Yaani wanataka kupoteza amani yetu, tuishi kwa kuhangaika hangaika."
Wazee hao walitumia mfano wa maisha ya kila siku kueleza athari mbaya za vurugu, huku wakigusa moja kwa moja maisha ya Watanzania wa hali ya chini.
"Hizi siku chache tu, sisi tusiokuwa nacho ilikuwa tuna matatizo. Kwa sababu sisi ununuzi wetu wa unga ni nusu kilo nusu kilo. Sasa usipopata unga, unapata shida kwa sababu maduka yamefungwa," alifafanua mzee huyo. "Unaweza ukawa na senti yako lakini duka limefungwa. Kwa hiyo sisi tuliteseka sana. Tunataka kuwaambia vijana wetu waliopo mitaani tuliona hali ilivyokuwa mbaya."
Kauli hii inatoa taswira halisi ya jinsi uvunjifu wa amani unavyovuruga biashara ndogo ndogo, kuwanyima wananchi wa kipato cha chini uwezo wa kujipatia mahitaji ya msingi.
Ujumbe mkuu kutoka kwa wazee kwa vijana wa leo ni kutumia akili timamu na kukataa ushawishi wa makundi mabaya.
"Mna akili timamu, msifuate vitu vya kuambiwa ambiwa na watu," alionya mzee Ally. "Haya makundi ya kushawishiwa na watu bila kufikiri yatawapoteza na kuleta tatizo katika amani yetu."
Maoni kutoka kwa wadau wengine yalisisitiza umuhimu wa kujiimarisha ndani kwanza kabla ya kuitafuta amani nje. "Moyo unaotafuta amani hauna nafasi ya chuki. Tafuta amani ndani kwanza," alisema Brainlight_Graphics.
Wadau wengi walisisitiza jukumu la vijana katika kulinda urithi huu wa utulivu. Mmoja ambaye mtandaoni alijitambulisha kama Youth_ambasador alieleza: "Amani ni nguzo ya maendeleo, tushikamane kwa upendo ili Tanzania ibaki kuwa kisiwa cha utulivu na matumaini."
Kupitia kauli iliyosambazwa na Chief Mkwawaa, Watanzania walikumbushwa: "Umoja ni Nguvu, Utengano ni Udhaifu!" Kauli hiyo iliendelea kwa kuwataka wananchi kumkataa kila anayejaribu kuleta kauli za uchochezi au kutumia udini, ukabila, au tofauti zozote kututenganisha. "Tudumishe: Amani, Upendo, na Umoja wa kitaifa!" ilimaliza kauli hiyo.
Aidha, Ronaldo_Bernadinho aliongeza kuwa: "Amani tuliyonayo ni tunu na alama ya taifa letu maana mataifa mengine yamekosa hii sifa na wanakuja kwetu, kwahiyo nitoe ushauri... tudumishe amani yetu ambayo ndo msingi wa maisha bora na sio tuanze kuishi kwa hofu."