` WITO KWA WATANZANIA KUTUMIA FIKRA CHANYA KULINDA AMANI

WITO KWA WATANZANIA KUTUMIA FIKRA CHANYA KULINDA AMANI

  

Viongozi, wachambuzi wa kijamii, na wadau wameungana kutoa wito kwa Watanzania wote kudumisha amani na umoja wa nchi, huku wakitahadharisha dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayolenga kuleta vurugu, hususan kuelekea mwezi wa Desemba. Kauli za wadau zinabainisha wazi kuwa, bila amani, hakuna mustakabali wa maendeleo, hasa kwa vijana.

Akizungumza kwa hisia, Bwana Shamte Mkali, alipongeza jitihada za uongozi wa nchi katika kuimarisha utulivu.

"Napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais ,Dkt. Samia Suluhu Hassan,kwani wakati ule hali ilipokuwa ngumu, wananchi wapo ndani wanasikilizia, Rais akasema neno, neno lile likatoa faraja nchi nzima. Kuanzia siku hiyo hali imekwenda vyema hadi leo," alisema Bwana Mkali, akisisitiza umuhimu wa kauli za kiongozi mkuu wa nchi.

Bwana Mkali pia alisisitiza umuhimu wa maridhiano kama msingi bora wa kutafuta amani na si vinginevyo.

 "Nchi hii ni yetu sote, ni lazima tuwe katika mshikamano... watu wakae wafanye mazungumzo, kwani shida ni nini? Taifa linaendelea na si kufanya fujo... vurugu hizo madhara sio kwa serikali tu, bali hata kwa wananchi na wale wanaoingia kuzifanya," alionya.

Wakati kukiwa na taarifa za uchochezi zikizunguka mitandaoni zikilenga kuleta vurugu Desemba 9, wadau wameonya umuhimu wa kuwa na fikra chanya na kukataa waziwazi wachochezi wanaojificha nyuma ya skrini.

Amani ni Tunu: "Amani tuliyonayo ni tunu na alama ya taifa letu maana mataifa mengine yamekosa hii sifa na wanakuja kwetu," alisema mdau mmoja katika mijadala ya kijamii, akitaka Watanzania kudumisha sifa hiyo.

Amani ni Ngao: Mdau mwingine alibainisha kuwa, "Amani ni ngao ya taifam,ikipotea kila mmoja huwa dhaifu. Vurugu huharibu utulivu wa taifa, biashara husimama, shule hufungwa na jamii hupoteza mwelekeo."

Katika mitandao imeoneshwa na taswira mbalimbali za uvunjifu wa amani ambao ndio adui mkubwa wa maendeleo ya vijana. Wakati amani ikivunjika na serikali inapambana na kuirejesha mara zote biashara na wawekezaji huondoka, ajira hupungua,elimu husimama: Shule hufungwa na vijana hukosa msingi wa kupata maarifa na badala ya kufanyakazi za maendeleo jamii huishi kwa wasiwasi.

"Hatuwezi kufurahia matunda ya maisha bila mbegu ya amani. Tupande mbegu hiyo leo," ni kauli inayotolewa kama ujumbe wa kuamsha Watanzania kuchukua hatua chanya.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464