
Dkt. Nchemba alitoa kauli hiyo yenye mkazo wa kizalendo alipokuwa akihutubia katika Kijiji cha Bombadia, Mjini Singida, ambapo aliwakumbusha wananchi kwamba miundombinu iliyojengwa nchini ni matokeo ya kodi zao, na si mali ya Serikali au vyama vya siasa.
Waziri Mkuu alibainisha wazi kuwa siyo utamaduni wa Watanzania kuchukiana, na kwamba chuki inayopandikizwa hivi sasa inatokana na makundi yenye maslahi binafsi.
"Wapo watu wanaowagombanisha Watanzania ili wapore rasilimali zilizopo. Nchi ni mali ya wananchi na mtu anapoiwasha moto, hamkomoi mtu mwingine yeyote zaidi yake mwenyewe," alisisitiza Dkt. Nchemba.
Alionya kuwa miundombinu hiyo iliyojengwa kwa jasho la wananchi inapaswa kulindwa, na kwamba kutojiepusha na uchochezi kunaweza kuharibu mali za umma, jambo ambalo linaweza kuathiri ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.
Katika hotuba yake, Dkt. Nchemba alikumbusha Watanzania kurejea kwenye misingi ya umoja na mshikamano.
Waziri Mkuu aliwahimiza vijana na wananchi kwa ujumla kuchukua hatua ya kulinda mali zao na amani yao wenyewe, akisisitiza kuwa, "Kila mtendaji afanye kazi kama nyakati zinavyohitajika."