` VETA KISHAPU YAANDIKA HISTORIA,YAFANYA MAHAFALI YA KWANZA HUKU IKITANGAZA FURSA MPYA

VETA KISHAPU YAANDIKA HISTORIA,YAFANYA MAHAFALI YA KWANZA HUKU IKITANGAZA FURSA MPYA

    Na Sumai Salum – Kishapu

Chuo cha Mafunzo Stadi (VETA) Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kimefanya mahafali yake ya kwanza ya wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi ngazi ya pili (Level II) tangu kuanzishwa kwake, tukio lililofanyika Novemba 14, 2025 katika viwanja vya chuo hicho kilichopo Kata ya Igaga.

Mgeni rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter N. Masindi, amewapongeza Walimu,Wahitimu na Wanafunzi wanaoendelea na masomo kwa juhudi na nidhamu waliyoionesha tangu walipoanza mafunzo yao.

Akizungumza katika mahafali hayo, Mhe. Masindi amesema ujuzi walioupata unatakiwa kuwa nyenzo ya kuwainua kimaisha na kuchangia maendeleo ya Taifa, huku akiwaelekeza kuzingatia misingi minne muhimu ya mafanikio ikiwa ni pamoja na Kumjua Mungu,Kuwa na watu kwenye maisha yao (ushirikiano),Kujali muda na Kuwa na nidhamu ya fedha.Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na mgeni rasmi Mhe.Peter MASINDI akizungumza kwenye mahafali ya kwanza ya Chuo cha Ufundi Stadi VETA Wilayani humo Novemba 14,2025 yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyoAmesisitiza kuwa serikali imeweka mikopo na fursa mbalimbali kwa vijana na wajasiriamali, hivyo wahitimu wanapaswa kufanya kazi kwa bidii mara baada ya kuhitimu ili kunufaika na fursa hizo.

Aidha, Masindi amesema mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kukuza uchumi kupitia viwanda vingi vitakavyochochea ajira na maendeleo ya wananchi mmoja mmoja. Amesema ujuzi walioupata chuoni uwe ni msingi wa mafanikio yao na kuwataka kutokata tamaa katika safari ya kujitegemea.

"Mjitunze muwapo mazingira ya utafutaji jiepusheni na makundi mabaya yatakayopelekea kuharibu mustakabali wa maisha yenu ya kesho mkumbuke familia zenu zinawategemea hakuna mwenye huruma na maisha yako zaidi ya wewe binafsi" amesisitiza

Sambamba na hayo Mkuu huyo wa Wilaya amekabidhi vyeti kwa wahitimu 42 waliohitimu mafunzo katika fani mbili—Umeme wa Majumbani na Ushonaji.Katibu Tawala Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Fatma H Mohammed akizungumza katika sherehe ya mahafali ya kwanza ya Chuo hicho Novemba 14,2025 yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo

Akitoa taarifa ya chuo, Mkuu wa Chuo cha VETA Kishapu, Tajiri Mollel, amesema chuo kilianza rasmi kutoa huduma Januari 22, 2024 kikidahili wanafunzi 45 katika fani mbili, 36 wa fani ya Umeme wa Majumbani na 9 wa Ushonaji. Hata hivyo, watatu kati yao walishindwa kuendelea kutokana na makosa ya kinidhamu.

Mollel amesema chuo kinakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa uzio, na akatoa wito kwa wazazi na walezi wa Wilaya ya Kishapu kupeleka vijana wao ili wapate mafunzo yatakayowasaidia kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukipatia chuo hicho vitendea kazi kwenye karakana nne, jambo lililosaidia kuboresha utoaji wa mafunzo.
Mkuu wa chuo Cha VETA Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Tajiri Mollel akizungumza katika sherehe ya mahafali ya kwanza ya Chuo hicho Novemba 14,2025 yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo"Pia tunazo shukrani zingine za kipekee kwa Mkurugenzi wetu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kutupatia gari kwa ajili ya kozi ya udereva itakayoanza kudahili wanafunzi wa fani hiyo ifikapo Januari mwaka 2026" ameongeza Mollel

Hata hivyo Veta Kishapu mpaka kufikia Januari 2026 itaendelea kutoka jumla ya fani 6 ikiwa ni pamoja na Umeme wa majumbani, Ubunifu,Ushonaji na Technolojia ya nguo,Ujenzi/uwashi, Uchomeleaji vyuma,Ufundi magari na Uhazili na Tehama.

Chuo cha VETA Kishapu ni miongoni mwa vyuo 29 vya Wilaya vinavyomilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa lengo la kusogeza huduma za elimu na mafunzo ya ufundi stadi karibu na wananchi ili kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi na uwezo wa kuchangia uchumi wa Taifa.Wahitimu 42 wa fani ya Umeme wa majumbani na Ushonaji Chuo Cha VETA Kishapu mkoani Shinyanga wakifurahia kwenye mahafali yao Novemba 14,2025









































































































Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464