` DKT LUZILA ATOA RAI KWA WANANCHI KUJENGA UTAMADUNI WA KUPIMA AFYA ZAO MARA KWA MARA

DKT LUZILA ATOA RAI KWA WANANCHI KUJENGA UTAMADUNI WA KUPIMA AFYA ZAO MARA KWA MARA



Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MGANGA Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dkt. John Luzila, ametoa wito kwa wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara, ili kutambua hali zao za kiafya na kupata ushauri wa kitaalamu mapema.

Ametoa rai hiyo leo Novemba 15, 2025 wakati wa kuhitimisha zoezi la upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza bure, lililofanyika kwa muda wa siku tano katika viwanja vya Zimamoto mjini Shinyanga.
Amesema katika kambi hiyo,malengo yalikuwa kufikia watu 500, lakini wamevuka lengo hilo baada ya wananchi kujitokeza kwa wingi zaidi ya miatano, na kwamba katika upimaji huo, watu 232 wamegundulika kuwa na shinikizo la damu, 55 matatizo ya sukari, 307 uzito uliokithiri, huku 27 wakigundulika kuwa na uzito wa chini ya kiwango.

“Natoa wito kwa wananchi kuanzia miaka 18 na kuendelea, wajenge tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kubaini mapema changamoto za kiafya na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu,” amesema Dkt. Luzila.
Ameongeza kuwa katika zoezi hilo pia wamefanikiwa kukusanya uniti 25 za damu salama, na kuwaomba wananchi kuendelea kujitokeza kuchangia damu kwa kuwa uhitaji bado ni mkubwa hususan kwa wajawazito na watoto.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupima afya, akiwamo Emmanuel Kayange, wamepongeza kambi hiyo kwa kuwasaidia kupata huduma muhimu na kujua hali zao za afya, huku wakihamasishwa kubadili mitindo ya maisha.

Zoezi hilo la upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza liliratibiwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, na lilianza Novemba 11 na kuhitimishwa leo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464