` MIHEMKO HAPANA, KIPAUMBELE NI MARIDHIANO

MIHEMKO HAPANA, KIPAUMBELE NI MARIDHIANO


Katika kile kinachoonekana kama msimamo wa kitaifa unaoongozwa na vijana, wito mkubwa umetolewa kwa kundi hili muhimu la Taifa kutambua umuhimu wa amani, kuachana na ushawishi wa mihemko binafsi, na kuweka nguvu zao katika kazi, kujenga uchumi, na kufanya maridhiano.

Vijana wanaojitambua wanasisitiza kwamba "Amani iwe ajenda Yetu" ili kulinda maendeleo tuliyonayo.

Vijana wametahadharishwa kwamba "tulikotoka ni kugumu na tunakoenda kulaini," wakisisitizwa kuwa wanapaswa "kuchapa kazi" badala ya kusikiliza mihemko inayoweza kuwarudisha nyuma.

Bw. Amir Jafary, fundi wa kutengeneza bodi za magari, akionyesha uzoefu wake, ameeleza bayana kuwa: "Kutokana na umri wangu, (naona) nchi hii ni nzuri. Tulikotoka na tunakoelekea mbele kuko zuri. Taifa limejitahidi tofauti na vijana waliozaliwa juzi."

Bw. Jafary alisisitiza kuwa mataifa yaliyo kwenye machafuko, kupata amani upya na kuendeleza maendeleo ni jambo gumu sana, kinyume na baadhi ya dhana kuwa machafuko ndio chanzo cha maendeleo.

Ujumbe wa msingi wa Desemba 9 na siku zijazo, umekuwa ni "Kataa uchochezi tujenge nchi yetu." Vijana wanakumbushwa kuwa maisha yao ya kila siku, biashara zao, miradi, na maendeleo yote yanapatikana kukiwa na amani.

"Amani ndio nguzo pekee inayotuwezesha kufanya kazi, kujifunza na kujenga familia zetu bila hofu," ilisomeka sehemu ya wito, ikisisitiza kuwa hakuna sababu ya kuruhusu upotoshaji uwapeleke kwenye "maandamano yasiyo na mwelekeo" au "vurugu zinazoweza kurudisha nyuma maendeleo."

Mshikamano wa vijana umeonekana kuwa ndio silaha kuu dhidi ya yeyote anayetaka kuvuruga utulivu wa nchi.

Vijana wanaojitambua wamepongeza juhudi za serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuweka kipaumbele kwa maslahi yao, hususan kwa kuunda Wizara kamili ya Vijana.

Bw. Jafary aliongeza kuwa uwepo wa Wizara hiyo ni mzuri, kwani sasa vijana wanaweza kueleza shida zao kwa watu wao.

Zaidi ya hayo, wito umetolewa kwa kufuata utaratibu wa maridhiano badala ya kukurupuka na kuleta vurugu.

"Suala la maridhiano nji mzuri. Kama kuna kero inatakiwa izungumzwe tukae sehemu moja tuangalie cha kufanya. Tunajua hii inafaida, vijana wasikurupuke."

Katika kulinda utulivu wa nchi, wazee wa kiroho, ikiwemo Maaskofu na Mashehe, wametakiwa kutumia majukwaa yao kuwajenga waumini katika dini na uzalendo, na kuachana na "makelele" yanayoweza kuhatarisha amani.

"Tanzania bila amani si Tanzania tunayojua. Tuchague utulivu," umemalizia wito wa vijana, wakisisitiza kuwa mshikamano wetu na uzalendo ndio dhamana ya maisha bora.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464