Majadiliano mbalimbali mtandaoni yameonesha msimamo imara wa Watanzania, hususan vijana, wa kukataa kurubuniwa kufanya vurugu, huku wakikazia umuhimu wa amani na utunzaji wa miundombinu ya Taifa.
Ujumbe huu umekuja wakati ambapo tahadhari imetolewa dhidi ya vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyoweza kujitokeza, ikitajwa moja kwa moja kuwa "Amani ndiyo kila kitu."
Wakitangaza uzalendo wao kwa vitendo, vijana wengi wamefanya wito wa pamoja wakisema: "Nchi hii ni yetu, tusikubali hata siku moja kuichoma nchi yetu wenyewe."
Katika mijadala hiyo, amani imetajwa kuwa ni "tunu na alama ya taifa letu," huku ikisisitizwa kuwa mataifa mengine yameikosa sifa hiyo na hivyo kuifanya Tanzania kuwa kimbilio na mfano bora. Wajadilianaji walisisitiza kuwa amani ndiyo "msingi wa maisha bora" na "nguzo ya maendeleo," na kwamba uzalendo ndiyo nguvu inayolijenga taifa kuwa imara.
"Tunapaswa kudumisha amani yetu ambayo ndio msingi wa maisha bora na sio tuanze kuishi kwa hofu," alisema mmoja wa wachangiaji, akionyesha wasiwasi juu ya athari za vurugu kwa makundi maalumu kama vile watoto, wazee, na wanawake.
Licha ya wito wa amani, mjadala huo uligusa moja kwa moja vitendo vya uharibifu wa miundombinu, ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa nchini. Ilibainika kuwa miundombinu kama vile barabara, taa, na mabasi ya mwendo kasi, ni "chakula kikuu Cha maendeleo yetu" na "fahari yetu kama Taifa/Jamii."
Vijana walikemea vikali vitendo vya wizi na uharibifu, wakitoa mfano wa watu wanaovunja na kuiba taa za barabarani au kuchoma basi la mwendokasi kwa kisingizio cha kudai haki.
"Mfano mtu unavunja na kuiba taa za barabarani eti unadai haki, unaiba taa hizo kweli ni haki au Wizi huo?" alihoji mchangiaji mmoja.
Mwingine alisisitiza athari za moja kwa moja za uharibifu huo kwa familia za Kitanzania: "Unapochoma mwendokasi unataka nini haki au? Haya umechoma kesho baba yako hajatoka kwenda kazini wewe hapo na wadogo zako hamuwezi kula tena," akifafanua jinsi vitendo hivyo vinavyoathiri mzunguko wa kiuchumi na maisha ya kila siku.
Ujumbe mkuu ulioibuka ni kwamba, ingawa kunaweza kuwa na changamoto zinazohitaji mabadiliko, "zipo njia za kutumia kufanya mabadiliko lakini siyo kwa kuchoma moto nchi unayoishi Watanzania."
Kutokana na msimamo huu imara, vijana wa Tanzania wamesisitiza haja ya kutambua kutunza na kulinda miundombinu yao, wakisisitiza kuwa uzalendo na amani ndio njia pekee ya kujenga Taifa imara.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464