.jpg)
Mjadala mkali kuhusu namna nchi za Kiafrika zinavyotangazwa duniani umeibuka kufuatia kauli za msanii na mfanyabiashara mashuhuri wa Kimarekani mwenye asili ya Afrika, Akon. Akizungumza kuhusu umuhimu wa 'Branding' (Kujitangaza) wa taifa, Akon amesisitiza kuwa vyombo vya habari na wasanii wana jukumu la msingi la kubadilisha simulizi hasi (negative narratives) zinazoelekezwa barani Afrika.
Kauli za Akon zinazosisitiza falsafa ya kibiashara ya "Dunia ni namna unavyojitangaza" zimetumika kutoa wito mpya kwa Watanzania na Waafrika kwa ujumla, hasa waandishi wa habari, kuacha mtindo wa "Hatutaki Tena" wa kupeperusha habari zenye madhara.
Akon, ambaye amejijengea himaya yake ya biashara na muziki kimataifa, anatoa muhtasari wa kibiashara unaoelezea kwa nini Marekani inaonekana yenye nguvu na ushawishi zaidi duniani.
"Hii Dunia ni namna unavyojitangaza. Ukijitangaza kwa ubaya utaonekana mbaya, ukijitangaza kwa uzuri utaonekana mzuri," anasema Akon.
Alieleza kuwa Marekani inajulikana kama nchi ya kwanza kujitangaza kwa uzuri, ambapo filamu zao zimetumia wahusika kama Superman na Batman kusimulia hadithi za ushujaa na uwezo wa kipekee. Kinyume chake, alidai kuwa filamu za Kiafrika kwa kiasi kikubwa zimeshindwa kuonesha ushujaa wa viongozi na mashujaa wa bara hili, kama vile Shaka Zulu.
Akon alitumia mfano wa matukio ya kiusalama kulinganisha namna Marekani na nchi za Afrika zinavyoshughulikiwa na kutangazwa kimataifa.
"Kuna Marekani kulikuwa na matukio zaidi ya 25,000 ya mauaji lakini Kenya kulikuwa na matukio mawili tu yaliyohusishwa na ugaidi. Lakini Kenya ilionekana ni hatari mpaka watu waliogopa kwenda," alieleza.
Alisisitiza kuwa jukumu hili linabebwa na vyombo vya habari vya Afrika, ambavyo kwa mujibu wake, "kukitokea tatizo vinakimbilia kutangaza mabaya na kutoa simulizi mbaya, wakati wenzetu hawafanyi hivyo." Hii inajenga picha hasi, au 'negative effect', ambayo inaathiri sekta za kiuchumi kama utalii na uwekezaji.
Wito kwa Waandishi wa Habari na Wasanii
Kama Akon anavyosema, jukumu la kutangaza nchi kwa uzuri linabebwa na:Vyombo vya habari,Wasanii,Waandishi,Wachezaji filamu, na wengineo.
Wito unaotolewa kwa waandishi wa habari wa Kitanzania na waendeshaji wa vyombo vya habari kukumbatia falsafa hii ya 'Branding' chanya. Badala ya kuzipa kipaumbele habari chache hasi na kuharibu taswira, wajikite katika kutangaza uzuri wa kipekee wa Tanzania: utamaduni, vivutio vya utalii, fursa za uwekezaji, na maendeleo ya kiuchumi na si waandishi wa habari wa vyombo vya kimataifa wanaoitangaza Afrika kwa kuweka mbele picha mbaya wakiwa na lengo la kudhalilisha badala ya kujenga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464