Waziri Mkuu Mhe. Mwigulu Nche
mba ametoa wito kwa Watanzania wote kutafakari na kuimarisha amani na utulivu, akisisitiza kuwa uhai na maisha ya kila mmoja yanategemea kuendelea kuwepo kwa utulivu nchini.
Kauli hiyo imepokewa kwa hisia kali na wananchi, huku wito mpya ukitolewa wa kuitumia teknolojia kama ngao ya kulinda umoja wa taifa.
Akitoa tahadhari kuhusu athari za uvunjifu wa amani, Mhe. Mwigulu alieleza kuwa nchi ina watu takribani milioni 62, ambapo kila mmoja ana ratiba na majukumu yake ambayo huathiriwa moja kwa moja na machafuko.
“Maisha yetu, uhai wetu unategemea Amani na Utulivu. Panapotokea uvunjifu wa amani, watu wengi wanapata mateso. Mama mjamzito anayetakiwa kujifungua atapata madhara makubwa kunapokea uvunjifu wa amani,” alisema Waziri Mkuu.
Alisisitiza kuwa amani si suala la hiari bali ni msingi mkuu wa maisha bora na maendeleo.
Wito wa Waziri Mkuu umeungwa mkono na wananchi, ambao kupitia majukwaa mbalimbali, wametahadharisha juu ya madhara ya migawanyiko na kutokuwepo kwa maridhiano, huku kauli moja ikitawala: "Amani ni msingi wa maisha."
Maoni kadhaa yaliyoonekana kuungwa mkono na wengi ni pamoja na:Tuungane kama Watanzania: "Kama Watanzania tuwe wamoja ili kuilinda Amani yetu.".Kazi na Utu: "Kazi Na Utu Tunasonga Mbele kuhakikisha Nchi inakuwa na Amani muda wote."Bila Amani hakuna maisha bora: Watu wengi walisisitiza, "Bila amani hakuna maisha bora."
Mwananchi mmoja aliyetambulika kama Bw. Makaranga, ambaye maoni yake yamekuwa yakienea, alipongezwa na wananchi wenzake kwa kusisitiza umuhimu wa maridhiano na kuacha jazba.
Katika nyakati za sasa za kidijitali, vijana na wadau wamependekeza Teknolojia itumike kama zana kuu ya kulinda amani na kukuza maendeleo.
"Teknolojia ndiyo injini ya Maendeleo na ngao ya Amani yetu. Tutumie zana za kidijitali kuleta ubunifu katika biashara, elimu, na afya, na wakati huo huo, tutumie mitandao yetu kueneza ukweli, umoja, na taarifa sahihi za kujenga, ili kulinda Utulivu wa nchi yetu. Tujenge Tanzania ya Kidijitali bila Machafuko."
Wito huu unaonyesha mwelekeo mpya wa kuhamasisha matumizi ya mitandao ya kijamii na zana za kidijitali katika kuunganisha Watanzania, kuongeza ajira, na kuzuia kuenea kwa taarifa za upotoshaji zinazoweza kutishia amani ya nchi.
Taifa lina wajibu wa pamoja, kuanzia katika ngazi ya uongozi hadi mwananchi wa kawaida, wa kulinda amani, huku msisitizo ukiwa kwenye umoja, maridhiano, na matumizi sahihi ya teknolojia.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464