` WITO WA MARIDHIANO WAPAA, WANANCHI WAONYWA JUU YA JAZBA INAYOTISHA AMANI YA TAIFA

WITO WA MARIDHIANO WAPAA, WANANCHI WAONYWA JUU YA JAZBA INAYOTISHA AMANI YA TAIFA

Suala la maridhiano nchini limeendelea kuchukua nafasi kubwa katika mijadala ya kitaifa huku mwananchi mmoja akisisitiza kuwa umoja na utulivu vinahitajika kulinda mustakabali wa nchi.

Kupitia mitandao ya kijamii, Hezron Shadrack Makaranga wa Kitonga ametoa wito mzito kwa Watanzania kujikita kwenye maridhiano kama msingi mkuu wa kudumisha amani, akionya kuwa jazba na migawanyiko ni tishio.

Katika maoni yake yaliyopokelewa kwa hisia mbalimbali, Makaranga alieleza kushangazwa na baadhi ya watu wanaobeza dhana ya maridhiano, huku akisisitiza umuhimu wake.

"Maridhiano ni jambo la msingi. Mimi nashangaa wengine wanabeza wengine sijui namna gani lakini maridhiano ni msingi mkubwa wa kuwezesha amani. Bila kufanya maridhiano, hatuwezi kufikia muafaka."

Bw. Hezron alitumia tukio la kihistoria la Zanzibar kama mfano halisi wa nguvu ya maridhiano, akirejelea matukio ya 2001.

"Nakumbuka mwaka 2001 lilipotokea tatizo kule Zanzibar yalifanyika maridhiano na baadae tukapata serikali ya maridhiano."

Alionya kuwa, "Jazba ikitawala, hatutafanikiwa," na kuongeza kuwa Watanzania wanapaswa kujikita katika kushughulikia matatizo yao wenyewe kwa utulivu.

Makaranga alimalizia kwa kutoa changamoto kwa vijana, akisisitiza kuwa ujenzi wa taifa unategemea juhudi zao wenyewe.

"Mustakabali wa vijana utatokana na vijana wenyewe."

Kauli hii inalingana na msisitizo wa viongozi mbalimbali, ikiwemo kauli ya hivi karibuni ya Waziri MkuuMwigulu Nchemba aliyeeleza umuhimu wa umoja wa Watanzania ili kuilinda Amani iliyopo, hasa wakati nchi inapopitia hatua mbalimbali za maendeleo na mabadiliko ya kisiasa. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464