` DIRA MPYA YA ULINZI WA TAIFA; MAANA HALISI YA MAELEKEZO YA DKT. MWIGULU KWA MTANZANIA WA KAWAIDA NA MWENYE USHAWISHI

DIRA MPYA YA ULINZI WA TAIFA; MAANA HALISI YA MAELEKEZO YA DKT. MWIGULU KWA MTANZANIA WA KAWAIDA NA MWENYE USHAWISHI

 

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, alihitimisha mazungumzo yake na wahariri wa vyombo vya habari kwa kutoa maelekezo mawili mazito kwa Taifa, ujumbe ambao unazidi mipaka ya siasa na unagusa moja kwa moja wajibu wa kiuchumi na kijamii wa kila Mtanzania.

Maneno haya yana maana tofauti na nzito kwa Mtanzania wa kawaida, na kwa viongozi na wafanyabiashara.

Mtanzania wa Kawaida Ndio Mlinzi Mkuu wa Taifa

Kwa Mtanzania anayejipatia riziki yake kwa jasho, maelekezo ya Waziri Mkuu yamefanya ulinzi wa Taifa kuwa jukumu la nyumbani, akisisitiza: "Tanzania si mali ya Serikali... Tuilinde nchi yetu."

Hii inamaanisha kuwa wajibu wa kulinda mali za umma, amani, na rasilimali za nchi hauko kwenye mikono ya Jeshi au Polisi pekee, bali ni jukumu la kila raia. Dkt. Mwigulu amesisitiza kwamba Amani inaanza kwenye kitongoji chako, akitoa onyo: "Hawa watu wabaya hawafikii tena kwenye nyumba za wageni, wanafikia kwa mtu mmoja mmoja."

Kauli ya Waziri Mkuu inamwomba Mtanzania wa kawaida awe mlinzi wa jirani yake kwa kutoa taarifa za wageni wasiofahamika. Kila mmoja anatakiwa "awe mlinzi wa mwenzake, kwa kujua kuwa huyo aliyemleta ni nani." Kwa kufanya hivyo, Mtanzania anakuwa anajilinda yeye mwenyewe na mali aliyoichangia kwa kodi.

Kundi Lenye Ushawishi Lipewe Kipaumbele Sekta Binafsi

Kwa upande wa viongozi, watumishi wa umma, na wafanyabiashara wakubwa, ujumbe wa Dkt. Mwigulu unahimiza mabadiliko ya mtazamo kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi.

Kwanza, Waziri Mkuu amewaondoa viongozi wa kisiasa katika dhana ya umiliki binafsi, akisema "Tanzania si mali ya chama cha siasa." Hii inamaanisha kuwa lengo kuu la wanasiasa wote linapaswa kulinda Taifa na si maslahi ya chama.

Pili, ameonya: "Hatutaushinda umaskini kama tutaamini kwamba sekta binafsi ni maadui." Huu ni mwito kwa Watumishi wa Umma kubadilisha mtazamo, kuona Wafanyabiashara kama washirika muhimu wa maendeleo, na kuacha dharau dhidi ya sekta hiyo.

Maelekezo kuhusu kuboresha mazingira ya Sekta Binafsi yanaambatana na hatua za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kumpa mkandarasi Mzawa miradi mikubwa. Hii inamaanisha kwamba mazingira yanaboreshwa ili wajasiriamali wa Kitanzania waweze kupata fursa kubwa, ambazo zitaajiri vijana wengi wa Kitanzania.

Ahadi ya Kulinda Rasilimali

Kwa kumalizia, Dkt. Mwigulu ametoa tamko la uhakika kwa wawekezaji na Watanzania wote: "Tutailinda Tanzania na rasilimali zake kwa gharama yoyote ile, watameza mate hadi yataisha." Huu ni ujumbe wa amani na usalama, unaohakikisha kuwa mali za nchi hazitapotea, na dhamira ya uovu dhidi ya rasilimali za taifa itakataliwa kwa nguvu zote.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464