` LUGHA ZA CHUKI NA UTAMADUNI WA KUDHALILISHA VIONGOZI HUSHUSHA UCHUMI WA TAIFA

LUGHA ZA CHUKI NA UTAMADUNI WA KUDHALILISHA VIONGOZI HUSHUSHA UCHUMI WA TAIFA

Ujumbe mkali umetolewa kwa umma wa Watanzania, ukisisitiza kuwa amani na mshikamano wa taifa uko hatarini kutokana na kuingizwa kwa lugha za chuki na utamaduni wa kudhalilisha viongozi kupitia majukwaa ya kidijitali.

Wasambazaji wa ujumbe huu katika majukwaa tofauti wamesema kwamba tabia hii mpya, inayoenezwa kwa kasi na kwa maslahi ya kifedha, inatishia kubomoa misingi ya umoja uliodumu nchini tangu enzi na enzi.

Waandishi wa ujumbe huo wamedai kuwa, baadhi ya watu wanaojihusisha na uanaharakati na biashara za mtandaoni wanatumika na watu wenye maslahi binafsi kuvuruga amani.

Wamesema wachochezi hao hawaishi nchini, bali ni wafanyabiashara wanaolipwa pesa nyingi ili kuvuruga uchumi wa taifa na kuingiza nchi kwenye machafuko.

"Kiukweli Watanzania tunahitaji amani, sio lugha za chuki zinazodhohofisha umoja na mshikamano wetu," ulisomeka ujumbe huo, ukiongeza kuwa hasara ya matendo haya inakwenda kuwaumiza wananchi wa kawaida pekee.

Wameonya kuwa, bila kuchukua hatua, nchi inaweza kutumbukia kwenye matukio mabaya yaliyozikumba mataifa mengine yaliyopitia machafuko, na kwamba maisha hayawezi kurudi kama zamani. Wamesisitiza kuwa wapo Watanzania waliokula njama na maadui kuingiza taifa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe ili nchi ifanywe shamba la bibi na kuachwa maskini.

Viongozi wa dini wametakiwa kutambua jukumu lao kubwa la kulikomboa taifa katika vurugu na kuirejesha amani, huku wakisisitiza kuwa maridhiano bila kumtanguliza Mungu hayawezi kufanikiwa.

Ujumbe huo umesihi Serikali kutokata tamaa, bali kutumia hekima, busara, uvumilivu, na subira kushughulikia hali ya sasa. Wameonya kuwa hakutapatikana mshindi kama wananchi na viongozi wa dini watakuwa mashabiki wa kuchochea vurugu badala ya kusimama kati kati ya pande zinazopingana ili kupata maridhiano.

Watanzania wengi waliotoa maoniu yao kwa ujumbe huo walikubaliana na wito huo, wakisisitiza umuhimu wa amani:

"Amani ni tunu tuilinde amani yetu," alisema mmoja.

"Amani tuliyonayo ni tunu na alama ya taifa letu," aliunga mkono mwingine, akiongeza: "Tulinde amani yetu ambayo ndo msingi wa maisha bora na sio tuanze kuishi kwa hofu."

Ujumbe mwingine ulisisitiza: "Tanzania ni kimbilio la wageni na hata wakimbizi kutoka Mataifa mbalimbali, tusipoilinda amani tutapoteza imani kubwa tuliyopewa ulimwenguni."

Wito umetolewa kwa kila Mtanzania kujitafakari, kutofuata mikumbo, na kutambua kwamba kila Mtanzania ana haki na wajibu wa kudumisha amani ya nchi yetu kwa wivu mkubwa sana.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464