
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, ametoa wito wa kutekelezwa kwa kasi kubwa, maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yanayolenga kurejesha haraka utoaji wa huduma za umma kwa wakazi wa Ilala kufuatia vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi.
Akizungumza na watendaji wa wilaya hiyo, DC Mpogolo alisisitiza umuhimu wa kurejesha hali ya kawaida, kuanzia katika miundombinu ya ofisi za umma.
"Tunapaswa kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kasi kubwa ya kuhakikisha tunarudisha utoaji wa huduma kwa Wana Ilala. Kwa pamoja tumedhamiria kujenga Ofisi zetu na tuweze kuwahudumia watu," alisema Mhe. Mpogolo.
DC Mpogolo alipongeza vikosi vya ulinzi na usalama kwa kazi yao ya kudhibiti hali ya usalama na kufanya Wilaya ya Ilala kuwa salama. Alieleza kuwa juhudi hizo zilifanikiwa kuzuia uharibifu zaidi wa mali za watu na mchakato wa uchaguzi.
"Tunavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuokoa baadhi ya mali na kuwakimbiza wale watenda maovu waliodhamiria kuteketeza mali za watu na kuharibu uchaguzi. Hawakufanikiwa," alisisitiza.
Alibainisha kuwa utendaji kazi wa vyombo hivyo ulikuwa wa hali ya juu na umehakikisha amani inarejea haraka.
Pamoja na pongezi hizo, Mkuu huyo wa Wilaya alitoa wito kwa watendaji wa serikali na wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vya usalama ili waweze kuendelea na kazi ya kuwatafuta na kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika na vurugu hizo.
"Vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na kazi. Naomba watendaji kutoa ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vya usalama kutoa ushirikiano. Tunataka kuhakikisha wale wote walioshiriki katika uharibifu wanabainika."
Akitoa maelekezo ya moja kwa moja, DC Mpogolo alimpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Elihuruma Mabelyana kwa kutoa agizo la kuharakisha ujenzi na ukarabati wa miundombinu yote ya utoaji huduma ya umma iliyoharibiwa wakati wa vurugu.
"Nampongeza Mkurugenzi wa Halmashauri,kwa kuelekeza miradi yote ya serikali, ofisi zote za serikali ziendelee kujengwa na nyingine kukarabatiwa kwa ajili ya kurejesha huduma za umma ... ile miradi yote ya serikali, ofisi zote za serikali ziendelee kujengwa ili wananchi waendelee kupata huduma," alieleza.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464