
Wiki chache baada ya ghasia na vurugu zilizofuatana na uchaguzi, Watanzania kutoka maeneo mbalimbali wamejitokeza kwa umoja kutoa tamko la dhati la kuahidi kuilinda amani, wakibainisha kuwa matukio hayo yaliwaacha na somo la maumivu.
Kauli za wananchi zilizosambaa mitandaoni zinaonyesha mwafaka wa kitaifa unaopita mipaka ya kijiografia: "Kutoka Arusha hadi Mbeya, kutoka Mwanza hadi Songwe, Watanzania wanasema kwa sauti moja: Amani ndiyo njia, na sisi ndio walinzi wake."
Miongoni mwa walioeleza athari za vurugu hizo ni Bi. Witness Rabson Nkini, mkazi wa Mvuti, Dar es Salaam, ambaye biashara yake iliathirika moja kwa moja. Witness alieleza jinsi uchafuzi wa amani ulivyosimamisha maisha yao na kuwalazimu kutumia fedha nyingi katika kununua vyakula.
"Kipindi cha uchaguzi kulikuwa na mtafaruku, kulikuwa na maandamano, ikatupelekea kufunga ofisi zetu. Kama mimi hapa nafanya saluni, tumekosa fedha. Tukikosa fedha tukalamzika kutumia fedha nyingi kununua vyakula," alieleza Witness.
Alisisitiza kuwa matukio hayo yamepelekea kupungua kwa amani si tu kwa watu wazima, bali pia kwa watoto wao, akitoa wito: "Tunaomba tuwe na amani na upendo. Wengine tunawatoto wanakosa amani."
Ushuhuda wa Witness na wengine unaakisi hali halisi ya Watanzania wengi ambao sasa wanaeleza kwamba, "Tumepitia maumivu, tumejifunza somo. Leo tunachagua amani, kwa ajili ya familia zetu, kazi zetu na mustakabali wa Tanzania."
Kauli hizi zimeungwa mkono na jumbe mbalimbali zinazosisitiza:
"Watanzania hili Ni somo tumejifunza tuilinde amani. Amani ni tunu yetu."
"Uchafuzi wa amani hauna faida. Tuungane kuilinda nchi yetu."
"Maandamano ni biashara, wachache inawalipa na kuwanufaisha zaidi huku wengi tukiumia kwa kupoteza kazi, biashara zetu na madhara mengine mengi."
Wananchi wengi wameahidi kuendelea kuienzi amani kama msingi wa maendeleo, huku wakihimiza: "Kesho bora ya Tanzania itajengwa kwa kuendelea kuenzi amani, kuvumiliana na kushirikiana."
Katika kuimarisha azma ya kudumu ya amani, kuna wito wa dhati wa kuwaepuka wale wote wanaoweza kuvuruga utulivu wa taifa. Ujumbe ulioenea unasema: "Tusitoe nafasi kwa watovu wa amani nchini mwetu kuja kuvuruga amani, upendo na mshikamano tulionao."
Wengi wamekubaliana kuwa "Amani si tukio, ni maamuzi ya kila siku. Tuanze leo, kwa maneno yetu, matendo yetu, na mioyo yetu."
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464