` VURUGU ZINATESA: WAFANYABIASHARA WASEMA OKTOBA 29 NI FUNZO

VURUGU ZINATESA: WAFANYABIASHARA WASEMA OKTOBA 29 NI FUNZO

 

Wito wa kulinda amani na utulivu umeendelea kutolewa nchini, huku wananchi wakielezea namna matukio ya vurugu yanavyoathiri maisha yao, na kusisitiza kuwa matukio yaliyotokea Oktoba 29 nchini yanapaswa kubaki kama somo la kudumu.

Akizungumza kwa hisia kali, Bi. Sassha Maluvanya, mfanyabiashara anayemiliki duka la dawa, alisema amani ilipotea kabisa katika kipindi hicho, na kusababisha hofu na mateso kwa jamii.

"Amani ilikuwa imepotea kwa sababu ilifika kipindi tumefunga maduka yetu. Sisi tunategemea maduka, lakini sasa ukifika nyumbani watoto unawalisha uji asubuhi, uji mchana, na usiku tunapika ugali kama uji na mboga kubwa maharage tu," Bi. Maluvanya alieleza.

Aliongeza kuwa, hali ya kufungwa kwa huduma muhimu ilitisha sana, ikieleza jinsi hata mahali pa kununua nyama palikuwa hakuna: "Mabucha yamefungwa, hakuna mahali pa kwenda kununua nyama. Kwa hiyo, hali ile iliyopita imetisha sana. Ilikuwa muda mfupi, siku nne tu, lakini ilionekana kama miaka minne kwetu."

Bi. Maluvanya alionyesha wasiwasi mkubwa kuhusu huduma za msingi za afya wakati wa vurugu. "Tulikuwa tunawaza, watu wakiumwa tutapata wapi dawa za kuwauzia manake hamtokii tunapata wapi? Tunateseka kabisa."

Mfanyabiashara huyo alisisitiza kuwa Watanzania wameumbwa katika hali ya amani na hawajazoea ugomvi, akiomba amani iendelee: "Tunapenda iendelee hii hali ya amani... kitu kinapojitokeza (vurugu) tunakosa raha kabisa. Tunaomba amani, Watanzania ni watu wa amani, kwa hiyo ugomvi unapotokea tunateseka."

Maoni yake yanaungwa mkono na hisia za wananchi mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, ambao wote wanakubaliana kwamba vurugu za Oktoba 29 zimeacha fundisho kubwa.

"Tanzania imejengwa kwa mshikamano. Tulichokiona Oktoba 29 kinapaswa kuwa somo, si maisha yetu mapya," ilisomeka moja ya kauli.

"Kama una akili timamu kwa vurugu za 29 lazima umejifunza kitu," alieleza mwananchi mwingine.

Vijana nao walijitokeza kutoa maoni, huku mmoja akisema: "Kama Kijana nimepata elimu na funzo kubwa kuhusu vurugu zile."

Wengine walisisitiza umuhimu wa amani kama nguzo ya taifa: "Amani ni nguzo ya maendeleo, tushikamane kwa upendo ili Tanzania ibaki kuwa kisiwa cha utulivu na matumaini."

Wananchi wametoa wito kwa vijana kusimama kidete kulinda amani, wakisisitiza kuwa umoja ni nguzo kuu ya taifa.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464