Wakati taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, mjadala mkali umeibuka miongoni mwa vijana kuhusu umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika upigaji kura. Mfumo wa kidemokrasia unasisitiza kuwa Kura yako ni haki yako ya msingi, na usipopiga kura utachaguliwa viongozi, lakini bado kuna kundi kubwa la vijana linaelekea kukaa kimya.
Hoja iliyoibuliwa hivi karibuni na mmoja wa vijana, Said Nassoro ambaye ana makazi yake Kawe.
"Kama nilienda kusimama foleni kujiandikisha daftari la kudumu, kwanini Oktoba 29 nisiende kupiga kura?" Swali hili linafungua mjadala kuhusu utofauti kati ya kujiandikisha na kupiga kura na kwanini vijana wanahitaji kukamilisha hatua ya mwisho.
Sababu za Vijana Kukaa Kimya
Licha ya uhamasishaji mkubwa kutoka kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na wadau wengine kuna wimbi mtandaoni linalohimiza vijana kutoshiriki uchaguzi wakimezeshwa taarifa za uongo kuhusu michakato ya uchaguzi.
Wachambuzi wa mitandaoni wanasema japo idadi ni ndogo lakini vijana wanaweza kirahisi kupotoshwa na taarifa za uongo kuhusu michakato ya uchaguzi, jambo linaloweza kuwafanya waamini kuwa upigaji kura hauna maana.
Nassoro anasisitiza kuwa kujiandikisha ni ishara ya kwanza ya utayari wa kiraia, lakini kukamilisha zoezi kwa kupiga kura ndio uamuzi mkuu unaohitajika.
"Kama ulikuwa na nia njema ya kuchagua kiongozi, kwanini ufanye safari ya nusu kwa kujitokeza kwenye Daftari, halafu ukatae kukamilisha kwa kutumia kura yako? Kura yangu ina maamuzi. Inasaidia kwenye mjadala mtandaoni. Badala ya kulalamika baada ya uchaguzi, ni bora kutumia sekunde chache kwenye sanduku la kura."
Kina anaungwa mkono na Joshua Atanazi, kijana mwingine, ambaye alisema: "Kundi la vijana lina idadi kubwa nchini na ndiyo lenye nafasi ya kufanya mabadiliko chanya kupitia kura zao. Usipopiga kura, kesho usilalamike."
INEC Yasimama Kidete
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inaendelea kuhimiza vijana na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi. Kaulimbiu yao inabaki: "UCHAGUZI MKUU OKTOBA 29, 2025. Kura Yako Haki Yako Jitokeze Kupiga Kura."
Kwa mujibu wa Tume, upigaji kura ni hatua muhimu ya kutimiza wajibu wa kiraia na ndio msingi wa kuwa na haki ya kuwawajibisha viongozi baada ya uchaguzi. Taasisi za dini nchini pia zimehimiza waumini kuombea taifa na kushiriki katika zoezi hilo la kidemokrasia kwa amani.
Uchaguzi huu unawaweka vijana katika njia panda: ama waache sauti yao ipotee kwa kukaa kimya, au waitumie kura yao kama kifaa cha kuamua nani anastahili kuongoza taifa kwa miaka mitano ijayo. Jibu la swali la Nassoro, kwa mujibu wa INEC na wadau, ni wazi: Usiache kura yako iishe kwenye foleni ya kujiandikisha.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464