` DIWANI WA ITWANGI LIDYA PIUS AMEFANYA MKUTANO WA HADHARA KUWASHUKURU WANANCHI,BAADHI YA AHADI AMEANZA KUTEKELEZA

DIWANI WA ITWANGI LIDYA PIUS AMEFANYA MKUTANO WA HADHARA KUWASHUKURU WANANCHI,BAADHI YA AHADI AMEANZA KUTEKELEZA

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

DIWANI wa Kata ya Itwangi wilayani Shinyanga Lidya Pius, amefanya mkutano wa hadhara wa kuwashukuru wananchi wa kata hiyo, kwa kumpigia kura nyingi za ushindi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, Mbunge wa Itwangi Azza Hillal Hamad, pamoja na yeye mwenyewe katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.

Mkutano huo umefanyika leo Januari 17, 2026 katika viwanja vya Shule ya Msingi Luhumbo, na kuhudhuriwa na viongozi wa taasisi mbalimbali za serikali, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), madiwani wa Itwangi pamoja na wananchi.
Akizungumza katika mkutano huo, Lidya amesema anatoa shukrani za dhati kwa wananchi kwa imani waliyoonyesha kwa kuwapigia kura nyingi za ushindi, huku akiahidi kuwa ahadi zote alizozitoa wakati wa kampeni zitatekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitano, na baadhi yake zikiwa tayari zimeanza kufanyiwa kazi.

“Leo nimekuja kusema asante kwa wananchi wa Itwangi kwa kumpigia kura nyingi za ushindi Rais Samia, Mbunge wetu Azza, pamoja na mimi Lidya kuwa diwani wenu, asanteni sana kwa kutupatia imani yenu, nasi tutawatumikia kwa vitendo, na baadhi ya ahadi mmeshaanza kuona utekelezaji wake,” amesema Lidya.
Amesema katika kipindi chake cha uongozi atakuwa diwani wa wananchi wote bila kujali itikadi za vyama, akisisitiza kuwa yupo tayari kupokea ushauri na maoni ya wananchi muda wote ,kwa lengo la kushirikiana kuleta maendeleo ya kata hiyo.

Aidha, ametoa rai kwa watumishi wa serikali waliopo Itwangi kujitoa kwa moyo mmoja katika kuwahudumia wananchi kwa uzalendo, huku akiwataka kuepuka matumizi ya lugha zisizofaa na tabia ya kudai fedha ili kutoa huduma.
Katika mkutano huo, Lidya ametaja vipaumbele vyake vya awali kuwa ni kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, hususan kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na shule, pamoja na kusukuma mbele upatikanaji wa umeme ngazi ya vitongoji, ambapo tayari vitongoji vitano vimeingizwa kwenye mpango wa umeme wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Vipaumbele vingine ni pamoja na ukarabati wa miundombinu ya barabara, ukamilishaji wa Zahanati ya Kidanda, ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Zahanati ya Zobogo, ujenzi wa nyumba za watumishi katika Zahanati ya Butini, ambako kwa sasa wauguzi hulazimika kulala katika baadhi ya vyumba vya zahanati, pamoja na kupunguza uhaba wa matundu ya vyoo, ukarabati wa vyumba vya madarasa na kuunga mkono michezo ili kuibua vipaji vya vijana.
Aidha, amewaomba pia wazazi wachangia chakula cha wanafunzi shuleni, ili wapate chakula, na kwamba yeye atatoa Mbegu za Alzeti hekal 20 kwenye mashamba ya shule, ili zilimwe kwa shule kupata mafuta na hata kuuza mafuta hayo na shule kupata fedha za kununua chakula, sababu zao hilo linastahili ukame kulingana na hali ya hewa kuwapo kwa mvua chache.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Edward Ngelela, amempongeza diwani huyo kwa kufanya mkutano wa kuwashukuru wananchi, kwamba ametambua thamani yao kwake, huku akimsihi awatumikie katika kuwaletea maendeleo.
“Nyota njema huonekana asubuhi, diwani huyu ni nyota njema kwa wananchi wa Itwangi, tegemeeni mvua ya maendeleo, na mmpatieni ushirikiano,”amesema Ngelela.

Mwenezi wa CCM Mkoa wa Shinyanga Richard Masele, amesema Lidya ni diwani mwenye maono, msikivu, mnyenyekevu, mchapakazi, na kwamba kila anapokutana naye muda wote yupo site kushungulikia matatizo ya wananchi, kwa kufika pia kwenye Ofisi za taasisi za serikali kuwasilisha kero zao.

“Wananchi wa Itwangi diwani mmepata, anapambana sana kushungulikia matatizo yenu, mimi ni shahidi, na baadhi utatuzi wake umeshaanza, ikiwamo kupelekwa umeme ngazi ya vitongoji,” amesema Masele.
Pia, ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wajiunge na bima ya afya kwa wote, ambapo Kaya ya watu sita ni sh.150,000 na watatibiwa kwa muda wa mwaka mzima.

Nao baadhi ya Madiwani wa Itwangi, akiwamo Mhandisi Jumanne Rajabu wa Kata ya Puni, kwamba watashirikiana na Diwani mwenzake ambaye ni jirani yake katika kusukuma maendeleo ya wananchi.

TAZAMA PICHA👇👇
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Edward Ngelela akizungumza.
Mwenezi wa CCM Mkoa wa Shinyanga Richard Masele akizungumza.
Mwenezi wa CCM wilaya ya Shinyanga Emmanuel Lukanda akizungumza.
Diwani wa Itwangi Lidya Pius akizungumza kwenye mkutano wa kuwashukuru wananchi.
Diwani wa Itwangi Lidya Pius akizungumza kwenye mkutano huo.
Diwani wa Itwangi Lidya Pius akizungumza kwenye mkutano. 
Diwani wa Puni Mhandisi Jumanne Rajabu akizungumza kwenye mkutano huo.
Diwani wa Ilola Richard Kisena akizungumza kwenye mkutano
Diwani wa Bukene Majaliwa Luhende akizungumza kwenye mkutano huo.
Mkutano wa kuwashukuru wananchi ukiendelea.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464