Na Johnson James, KISHAPU
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amewataka mamalishe wote wilayani Kishapu na mkoa mzima kwa ujumla kuachana na matumizi ya nishati chafu kama mkaa na kuni, na kuanza kutumia nishati safi ili kulinda mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mhe. Mhita alitoa wito huo Januari 10, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika Kata ya Maganzo, Wilaya ya Kishapu.
“Shinyanga ni miongoni mwa mikoa inayokumbwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo ukosefu wa mvua hasa hapa Kishapu. Hii inatokana na uharibifu wa mazingira unaochangiwa na matumizi ya nishati chafu. Nawaomba mamalishe waanze kutumia nishati safi ili tusaidiane kutunza mazingira yetu,” alisema RC Mhita.
Ameongeza kuwa moja ya njia muhimu ya kukabiliana na ukame ni wananchi kupanda miti kwa wingi, akisisitiza kuwa miti si tu inapendezesha mazingira bali pia husaidia kurejesha mvua na kuimarisha mzunguko wa maji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, alimhakikishia Mkuu huyo wa Mkoa kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi kwa haraka na ufanisi.
Kampeni ya matumizi ya nishati safi ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kulinda mazingira na kuboresha afya ya wananchi, hasa wajasiriamali wadogo kama mamalishe.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464




