` POLISI WAKEMEA MATUMIZI MABAYA YA MTANDAO KULETA HOFU

POLISI WAKEMEA MATUMIZI MABAYA YA MTANDAO KULETA HOFU

 

Na Mwandishi wetu

Jeshi la Polisi nchini limetoa onyo kali kwa kundi la watu wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kusambaza chuki, taharuki, na propaganda za kuvuruga amani, likisisitiza kuwa vitendo hivyo ni uhalifu wa wazi na si uhuru wa maoni.

Akizungumza kwa msisitizo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamanda David Misime, alitoa kauli thabiti akisema, "Amani ya nchi yetu ni tunu isiyopaswa kuwekwa rehani kwa jazba au tamaa za wachache wenye nia ovu."

Kamanda Misime alieleza kuwa Jeshi la Polisi limebaini ongezeko la tabia za kiuhalifu zinazofanyika kupitia majukwaa ya mtandaoni, akizitaja kama:Kuhamasisha vurugu na maandamano yasiyo halali,Kueneza upotoshaji wa taarifa na chuki miongoni mwa wananchi,Kuvunja misingi ya sheria, maadili, na utamaduni wa Kitanzania.

"Tunawakumbusha Watanzania wote kuwa hakuna aliye juu ya sheria. Ujumbe wowote wa chuki, uchochezi, au ule unaolenga kuvuruga amani ya nchi yetu utashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za nchi. Huu si uhuru wa maoni, huu ni uhalifu," alikariri Kamanda Misime.

Akitoa onyo la moja kwa moja kwa wale wanaojihusisha na uhalifu huo, Kamanda Misime alisisitiza kuwa operesheni ya kuwakamata inaendelea.

"Kwa wale wanaoendelea kutumia mitandao kueneza vurugu na uongo, wajue wazi kuwa Sheria Ipo Macho, na muda wao ni mdogo. Jeshi la Polisi litaendelea kuhakikisha kuwa wote wanaojihusisha na uhalifu huu wanachukuliwa hatua za kisheria bila upendeleo," alisema.

Mwisho, msemaji huyo wa polisi alitoa wito kwa wananchi wote wenye mapenzi mema na taifa lao kuwa walinzi wa amani.

"Tunaiita jamii iwe sehemu ya suluhisho. Tuikatae jamii ya ujumbe wa chuki. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kulinda utulivu wa nchi yetu na kuilinda familia yake dhidi ya machafuko yanayochochewa na watu wachache. Watanzania tuilinde amani yetu, tuheshimu sheria, na tukatae upotoshaji wa mitandaoni," alisema Kamanda Misime.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464