Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Patrobas Katambi, amewakilisha wananchi wa Jimbo hilo mbele ya Mgombea Urais wa CCM, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwasemea kuhusu haja ya kufufuliwa kwa Kiwanda cha Tanganyika Packers kilichopo Old Shinyanga na Chama Kikuu cha Ushirika (SHIRECU) ili kuwawezesha wananchi kunufaika na shughuli za kilimo na kuinuka kiuchumi.
Katambi amesema hayo leo Oktoba 11,2025, katika mkutano wa kampeni wa Rais Dkt. Samia uliofanyika katika Uwanja wa CCM Kambarage, uliolenga kunadi sera na Ilani ya CCM kwa wananchi wa Shinyanga.
Amesema,Shinyanga imepiga hatua kubwa kimaendeleo hasa kwa utawala wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,na kwamba wanaomba kiwanda cha Tanganyika Packers kilichopo Oldshinyanga kifufuliwe pamoja na kukifufua Chama Kikuu cha Ushirika (SHIRECU)ambacho kilikuwa ni mkombozi kwa Mkulima.
“Mheshimiwa Mgombea Urais hapa Shinyanga tunatatizo la Kiwanda cha Tanganyika Packers, tunaomba Mheshimiwa kifufuliwe pamoja na Chama Kikuu cha Ushirika SHIRECU ili kuongeza mzunguko wa fedha na kuinua uchumi wa wananchi,”amesema Katambi.
Aidha,ametaja mafanikio ya miaka minne ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika Jimbo la Shinyanga Mjini,kwamba amekamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa,ukarabati Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, ujenzi wa Vituo vya Afya vipya vinane na upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa.
Amesema pia Rais Samia amejenga Uwanja wa Ndege Ibadakuli,Miundombinu ya Barabara,Madaraja na sasa anajenga Standi Kuu ya Mabasi ya Kisasa na ujenzi wa Lami kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Ameongeza kwa miaka hiyo minne katika Sekta ya Elimu amejenga Shule mpya 11 za Sekondari 5 na Msingi 6, huku kwa upande wa Sekta ya Maji ametoa ten ash.bilioni 195 na asilimia 94 ya wananchi wanapata maji safi na salama na kati ya Vijiji 3 vilivyosalia kupata Maji kati ya 17 vinakwenda kupata maji.
Amempongeza Rais Samia kwa kuendelea kuwezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo mbalimbali, pamoja na kutoa ajira kwa vijana zaidi ya milioni 884 kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ya kimkakati.
“katika Jimbo hili la Shinyanga Mjini Rais Samia amefanya mambo makubwa sana ya maendeleo haya ambayo nimezungumza ni machache tu, nikisema yote tutakesha hadi asubuhi,”amesema Katambi.
Naye Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, akizungumza kwenye mkutano huo,amemuhakikishia Katambi kwamba, SHIRECU wanakwenda kuifufua na Rais ameshatoa maelekezo ya kufanya tathimini ya kulipa madeni yote ambayo inadaiwa SHIRECU na watakipatia sh.bilioni 1.3 ili kufufua Kiwanda Chao cha kuchambua Pamba kilichopo Mhunze Kishapu.
Mgombea Urais kupitia CCM Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,amesema maombi mapya yote ambayo yameombwa ameyapokea na watayafanyika kazi.
Pia,amewaomba wananchi wa Shinyanga kwamba siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, wajitokeze kwa wingi kupiga kura na Kumchagua pamoja na Wabunge wote wa CCM na Madiwani.
TAZAMA PICHA👇👇
Mgombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CCM Patrobas Katambi akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais,Rais Dkt Samia Suluhu Hassan mkoani Shinyanga.

Mgombea Urais kupitia CCM,Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, akimpatia kitabu cha Ilani Mgombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi.
Mgombea Urais kupitia CCM,Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, akimpatia kitabu cha Ilani Mgombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464