Edwin Soko atoa tathimini ya utendaji wa Vyombo vya habari kwenye kampeni
Mwandishi wetu Mwanza
Mwandishi wa habari Mwandamizi na Mtetezi wa haki za binadamu Edwin Soko amesema kuwa, mazingira ya utendaji kazi wa Vyombo vya habari kwenye mikutano ya kampeni za wagombea yamekuwa rafiki kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Soko amesema hayo kwenye mahojiano na Vyombo vya habari Leo Jijini Mwanza juu ya tathimini ya utendaji kazi wa Vyombo vya habari kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025
" kuanzia Agosti 28 , 2025 hadi kufikia sasa hatujapata taarifa zozote za madhila Kwa Vyombo vya habari au waandishi wa habari yeyote yule hali inayoashiria kuimarika Kwa usalama wa Waandishi wa Habari na haki ya waandishi wa habari kufanya kazi bila kubuguziwa wakati huu wa kampeni za wagombea kwenye ngazi za Urais , Ubunge na Udiwani" Alisema Soko.
Soko pia aliongeza kuwa, amekuwa akifuatilia taarifa za utendaji kazi wa Vyombo vya habari tangia kampeni zianze Agosti 28 na kushuhudia uwajibikaji mkubwa wa waandishi wa habari pasipokuwa na vikwazo vyoyote vya kupata taarifa toka Kwa wagombea tofauti na kampeni za miaka ya nyuma.
Vile vile Soko amevipongeza Vyombo vya habari, waandishi wa habari na wadau wote wa uchaguzi likiwemo Jeshi la Polisi kwenye kuhakikisha vyombo vya habari na waandishi wa habari wanakuwa salama kwenye kampeni za uchaguzi za Mwaka 2025
" Mimi naamini uhuru wa demokrasia unaanzia kwenye uhuru wa Vyombo vya habari hivyo natoa rai kwa Vyombo vya habari kuendelea kufanya kazi kwa weledi ili kuandika habari za ukweli zinazolenga kuimarisha Umoja na mshikamano wa Taifa letu, pia nashukuru Wizara ya Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo chini ya Waziri Palamagamba Aidan Kabudi na Katibu Mkuu Gerson Msigwa kwa kuwa karibu na wadau wa kisekta hasa wakati wa changamoto zinapotokea zinazowahusu waandishi wa habari" Alisema Soko.
Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, vyama vya siasa 18 vinashiriki kampeni za uchaguzi Mkuu huku vyama vya siasa 17 vikisimamisha wagombea kwenye ngazi ya Urais .
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464