` WAZIRI RIDHIWANI KIKWETE AWASILI MBEYA KUKAGUA MAANDALIZI YA KILELE CHA MWENGE WA UHURU 2025

WAZIRI RIDHIWANI KIKWETE AWASILI MBEYA KUKAGUA MAANDALIZI YA KILELE CHA MWENGE WA UHURU 2025

 

📍Mbeya 9 Oktoba, 2025

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, amewasili jijini Mbeya kwa ziara ya kikazi kukagua maandalizi ya sherehe za Kilele cha mbio za mwenge wa Uhuru mwaka 2025. 

Katika kipindi hiki cha kuelekea kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, kutafanyika pia maonyesho ya wiki ya Vijana kuanzia tarehe 8 hadi 14 Oktoba 2025. Maonyesho hayo yanatarajiwa kuwakutanisha vijana kutoka sehemu mbalimbali, taasisi za Serikali, Sekta binafsi, mashirika ya maendeleo na wajasiriamali, kwa lengo la kuonyesha kazi na huduma zinazolenga kuwawezesha vijana kiuchumi, kielimu na kijamii. Wiki hii ya vijana inalenga kuwa jukwaa muhimu la kusherehekea mafanikio ya vijana, kuibua vipaji na kujadili changamoto pamoja na fursa zinazowahusu vijana wa Tanzania.
Aidha, ndani ya Wiki ya Vijana, kutafanyika Kongamano Kubwa la Taifa la Vijana litakalowakutanisha takribani vijana 1,500 kutoka maeneo mbalimbali ya nchi. Kongamano hilo linalotarajiwa kufanyika tarehe 13 Oktoba 2025, litaangazia mada mbalimbali zinazohusu maendeleo ya vijana, ajira, ujasiriamali, matumizi ya teknolojia, ushiriki wa vijana katika siasa na uongozi, pamoja na umuhimu wa mshikamano wa kitaifa. Mgeni rasmi katika kongamano hilo anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye atazungumza na vijana kuhusu nafasi yao katika mustakabali wa taifa.

Shughuli zote hizi zitahitimishwa na sherehe kubwa ya kilele cha mbio za mwenge wa uhuru zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba 2025 jijini Mbeya.

 Hafla hiyo itahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, huku mgeni rasmi akiwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kilele hicho kinatarajiwa kuwa sehemu ya maadhimisho ya mafanikio ya mwenge huo wa kitaifa ambao huwahimiza Watanzania kuhusu uzalendo, umoja, maendeleo na uwajibikaji katika jamii.

Katika ziara yake ya ukaguzi, Waziri Ridhiwani Kikwete alipata nafasi ya kutembelea maeneo ya maonyesho, kukagua maandalizi ya kongamano pamoja na kukutana na wananchi walioko katika maeneo hayo. Akiwa ameambatana na viongozi wa mkoa na wilaya, Ridhiwani alieleza kuridhishwa kwake na hatua za maandalizi na kuwapongeza waandaaji kwa kazi kubwa inayoendelea kufanyika ili kuhakikisha kila jambo linaenda kwa ufanisi mkubwa.

Akizungumza na wananchi wa Mbeya na Watanzania kwa ujumla, Waziri Kikwete alisema: “Nimepata fursa ya kukagua maandalizi ya shughuli hizi muhimu kwa Taifa letu na kukutana na wananchi wa Mbeya. Nimewaalika na ninawakaribisha Watanzania wote kushiriki kwa wingi. Karibuni sana Mbeya tusikilize na tujifunze kutoka kwa Mwenge wa Uhuru, ni nini umeona safari hii.”

Kama yalivyo maadhimisho ya miaka iliyopita, Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 unaendelea kubeba ujumbe mzito kwa Taifa. Safari yake kupitia mikoa yote inaleta taarifa za miradi ya maendeleo, changamoto za kijamii, mafanikio ya sekta mbalimbali pamoja na kutoa mwanga wa matumaini kwa Watanzania wote. Mbeya, ikiwa mwenyeji wa kilele cha sherehe hizi, inatarajiwa kuwa kitovu cha uzalendo, mshikamano na dira ya maendeleo ya vijana wa Tanzania.

#MwengeWaUhuru2025 #MbeyaYaMaendeleo #WikiYaVijana #TanzaniaYangu

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464