` MAGEREZA SHINYANGA YAANZA KUTUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

MAGEREZA SHINYANGA YAANZA KUTUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA



Na Mwandishi Wetu,SHINYANGA

Jeshi la Magereza mkoani Shinyanga,limeanza kutumia nishati safi ya kupikia kwa wafungwa,huku likipiga marufuku matumizi ya kuni ndani ya gereza.

Ofisa wa Dawati la Jinsia na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dk. Joseph Sambali,akizungumza
leo Septemba 23,2025 katika uzinduzi wa mradi huo uliofanyika Gereza Kuu la Shinyanga, amesema mkataba wa mradi wa usambazaji wa nishati safi ulisainiwa Septemba 13, 2024 na kugharimu Sh. bilioni 35.2 kwa muda wa miaka mitatu.
Amesema mradi huo unatarajiwa kusambaza mitungi 15,126 ya kilo 15 na pia kusambaza mkaa mbadala katika magereza mbalimbali.

“Tani tano za mkaa mbadala zimepelekwa Gereza la Shinyanga na zingine tano Kahama,pia tumetoa majiko banifu, mashine ya kutengeneza mkaa mbadala, mfumo wa biogas na mfumo wa EPG kwa ajili ya kupikia,” amesema Dk. Sambali.
Kwa upande wake,Mkuu wa Gereza wilaya ya Shinyanga Kamishina Msaidizi wa Magereza, Martin Kunambi, amesema gereza hilo limeanza kutumia nishati mbadala tangu Januari mwaka huu na kwamba chakula cha wafungwa wote sasa hupikwa kwa mkaa mbadala.

“Hapa Shinyanga tuna wafungwa 263, wote wanapikiwa kwa kutumia mkaa mbadala. Kuni haziruhusiwi kabisa,ukiingiza kuni ni sawa na kuingiza sigara – ni marufuku,” amesema Kunambi.

Naye mwakilishi wa kampuni ya Oryx Gas, Gipson Roggers, aliwafundisha askari magereza namna ya matumizi sahihi ya jiko la gesi pamoja na kujua kiasi cha gesi kilichobaki kwenye mtungi.
Mgeni rasmi, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REA), Ahmed Chinemba, amewataka wadau wote wa sekta ya nishati kushirikiana kupunguza matumizi ya nishati chafu.

“Jumla ya watumishi wa Magereza 221 wamekabidhiwa mitungi ya gesi ya kilo 15 na majiko ya sahani mbili. Mitungi yote ipo hapa na tunakabidhi leo,” amesema Chinemba.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464